Hali hiyo inasababishwa na idadi kubwa ya wakimbizi walio katika Kambi za Nyarugusu, Kagunga na Uwanja wa Lake Tanganyika.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali Mstaafu Issa
Machibya anasema katika Kambi ya Kagunga, iliyo uwanda wa Pwani ya Ziwa
Tanganyika kuna watoto 75,000, wanawake 6,000 na wanaume 7,000 ambao
wanahitaji maji, chakula na malazi.
“Hali ni mbaya sana kuna idadi kubwa ya wakimbizi,
wote wanahitaji kula, kulala na kutibiwa wanapougua,” anasema Kanali
Machibya.
Hata hivyo, takwimu halisi za idadi ya wakimbizi
walio katika kambi hizo inatatanisha kwani Shirika la Umoja wa Mataifa
la Kuhudumia Wakimbizi(UNHCR), linasema kuwa idadi ya wakimbizi katika
kambi zote ni 49,388 kwa sasa, huku kukiwa na tetesi kuwa baadhi
hawajulikani walipo.
Wakati huo huo, Ofisa Uhamiaji katika mpaka wa
Kambi ya Kagunga, Albert Jeremiah anasema tangu Aprili 29, wakimbizi
zaidi ya 90,585 wamesajiliwa kwenye kambi hiyo na baadhi wameelekea
Nyarugusu.
Jeremiah anasema kwa siku moja, meli za MV Liemba
na Mv Malagarasi hubeba wakimbizi 1800 na kuwapeleka Uwanja wa Lake
Tanganyika.
Walazwa vitanda vya miti, 3993 waathirika kwa kipindupindu
Idadi kubwa ya wakimbizi, imesababisha mlipuko wa
ugonjwa wa kipindupindu ambapo takwimu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma, Dk Leonard Subi, zinaonyesha kuwa hadi sasa kuna jumla
ya wagonjwa 3993. Kati ya wagonjwa hao, 25 ni Watanzania.
Saa 10:35 jioni wakati Mwananchi ilipoingia ndani
ya Kambi ya Nyarugusu, ilikuta kuna wagonjwa wa kipindupindu na kuhara
wakipewa chakula chao cha mchana, ambacho ni ugali na maharage huku
ikielezwa kuwa huo ndiyo mlo wa mwisho kwa siku hiyo, baada ya kunywa
uji asubuhi.
Ndani ya wodi hiyo kumefurika wagonjwa, wengine
wakiwa wamelala chini na wachache walio mahututi wakiwa wamelazwa kwenye
vitanda vya miti.
Mganga anayehudumia wagonjwa wa kipindupindu
katika kambi hii kubwa ya Nyarugusu, Dk Lawrence Mhina anasema hadi sasa
kambi hiyo ina wagonjwa 115 wanaotibiwa.
Hata hivyo, Dk Subi ameagiza dawa za malaria aina ya Alu, ili zipelekwa katika kambi hizo na kwamba kuna kiasi cha kutosha cha dawa kwa wakimbizi wote.
Hata hivyo, anasema kuwa tangu wakimbizi kutoka Burundi waanze
kuingia nchini mapema mwezi uliopita, mpaka sasa hospitali hiyo imetibu
wagonjwa zaidi ya 500 wa kuhara na kipindupindu.
“Takwimu hizi za wagonjwa zinapanda na kushuka,
lakini mara nyingi tunapokea wagonjwa wengi usiku, wakati ambapo
wakimbizi kutoka Kagunga na Uwanja wa Lake Tanganyika huletwa kwa
mabasi,” anasema
Anabainisha kwamba changamoto kubwa katika kambi
hiyo ni idadi kubwa ya wagonjwa, vyumba vichache vya kuwaweka, uhaba wa
vitanda, mashuka na wahudumu wa afya.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) nchini,
Dk Rufaro Chatora anasema kuwa shirika lake litaongeza wahudumu wa afya
na misaada ya dawa kwani huenda hali ikawa mbaya zaidi kwa sababu
wakimbizi bado wanamiminika kutoka Kagunga.
“Lazima tuhakikishe tunazuia maambukizo mapya,
tuangalie uwezekano wa kuepusha watu kuambukizwa wakati wanaposafirishwa
kutoka kambi moja kwenda nyingine,”anasema
Dk Chatora anasema kuwa WHO itahakikisha dawa
zinapatikana kwa wingi katika maeneo yote yaliyoathiriwa na kipindupindu
na malaria.
“Huenda malaria nayo ikawa tatizo kubwa kwa sababu hawa watu wanalala nje na wanaumwa na mbu, “ anabainisha.
Hata hivyo, Dk Subi ameagiza dawa za malaria aina ya Alu, ili zipelekwa katika kambi hizo na kwamba kuna kiasi cha kutosha cha dawa kwa wakimbizi wote.
Wakati huo huo, kipindupindu katika Kambi ya Kagunga kimeathiri watu 1984, huku kukiwa na wagonjwa wapya 109 mpaka sasa.
Daktari wa Wizara ya Afya anayesimamia kambi hiyo,
Cyst Mosha anasema kwamba ingawa wagonjwa wanapata tiba na kuhudumiwa,
lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa chakula.
“Wagonjwa wanatibiwa, lakini hawana chakula cha
maana cha kuwapa nguvu, matokeo yake wanajikuta wakila vidonge vya
virutubisho kama chakula,” anasema.
Wagonjwa, hata wasio wagonjwa katika kambi hiyo
hujikuta wakikosa chakula kwa zaidi ya wiki, hali inayowasababishia
wengine kuzimia na kutundikiwa maji ya ‘glucose’ ili kuwapa nguvu.
No comments:
Post a Comment