Mkutano huo wa 20 wa Bunge la 10 ni wa mwisho
katika uhai wa chombo hicho cha kutunga sheria kabla ya kuvunjwa,
kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa
na Ofisi ya Bunge na Rais Jakaya Kikwete, zilieleza kuwa tayari
makubaliano yamefikiwa baina ya Bunge na Serikali ili kuwezeshwa
kufikishwa miswada hiyo katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Tano wa Chama cha Walimu
Tanzania (CWT), juzi usiku, Rais Kikwete alisema makubaliano hayo
yamekwishafanyika na miswada itakayojadiliwa mmojawapo ni wa kuanzishwa
tume ya utumishi ya walimu, ambayo inawezesha walimu nchini kuwa na
chombo kimoja cha kuwasimamia.
“Tayari tumezungumza na Spika wa Bunge na
tumekubaliana katika kikao kinachoendelea kitaongezwa siku 10 ili
kuwezesha kumaliza shughuli za serikali ikiwamo miswada,” alisema.
Chanzo kingine cha habari ndani ya Serikali
kilieleza kuwa moja kati ya miswada itakayowasilishwa na Serikali ni
pamoja na marekebisho ya sheria ya uchaguzi pamoja na muswada wa sheria
ya vyombo vya habari. Sababu nyingine inayotajwa kuhusu kuongezwa muda
kwa Bunge hilo ni Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ambao ndiyo wenye jukumu
la kuchagua mgombea urais wa chama hicho, ambao utafanyika kwa siku
mbili kuanzia Julai 11 hadi 12.
Wabunge wote wa CCM ni wajumbe wa mkutano huo,
hivyo kama Bunge litavunjwa Juni 27, 2015 watapoteza sifa za kuwa
wajumbe wa mkutano huo.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu chama hicho tawala kuhusishwa na nyongeza
ya siku za Bunge hilo alisema, “Huo ni upuuzi mwingine sasa. Vikao vya
CCM vimepanga ratiba kabla hata ya huo uamuzi wa Bunge unaousema. Hakuna
ukweli katika hilo.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), Jenista Mhagama alipoulizwa kuhusu suala hilo alishindwa
kukubali wala kukataa na kutaka atafutwe Katibu wa Bunge.Tayari Chama
cha Wamiliki wa vyombo vya Habari Tanzania (Moat), kimeunda timu maalumu
itakayokwenda bungeni kuwashawishi wabunge wasiupitishe muswada wa
sheria wa vyombo vya habari baada ya kubaini umejaa kasoro.
Muswada huo ulioandaliwa na Serikali ulitakiwa
kuwasilishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge kwa hati ya dharura bila
mafanikio na tayari Rais Kikwete amesema atausaini kabla hajaondoka
madarakani.
Naibu Spika, Job Ndugai alipoulizwa alisema: “Hilo
jambo bado hatujakaa katika kamati ya uongozi kulijadili vizuri. Bado
hatujajua Serikali inaleta miswada gani. Ila pamoja na hayo, hicho kitu
(kuongeza muda) kitakuwapo.”
Aliongeza, “Unajua mikutano ya Bunge huwa ni 20
tu, bado hatujajua hicho kikao kitakachokuja kitaitwaje. Jambo hili bado
ni bichi sana na huko nyuma hatujawahi kuwa na kitu kama hiki.
No comments:
Post a Comment