Tukio hilo linafanya idadi ya wanajeshi wa
Tanzania waliouawa nchini humo kufikia watatu baada ya askari mwingine,
Khatibu Mshindo kuuawa Agosti 2013 katika shambulio la bomu lililofanywa
na waasi wa kikundi cha M23 kwenye Mji wa Goma ulioko Mashariki mwa
DRC.
Wakati Mshindo, ambaye alikuwa miongoni mwa askari
wa Tanzania wanaounda Jeshi la Umoja wa Mataifa akifikwa na mauti,
wapiganaji wengine 10 walijeruhiwa.
Msemaji wa Mpango wa Kulinda Amani wa Umoja wa
Mataifa DRC (Monusco), Felix Basse alikaririwa na Shirika la Habari la
AFP akisema mashambulizi ya juzi yalifanyika katika Kijiji cha Kikiki
kilichoko kilomita 37, kaskazini - Mashariki mwa Mji wa Kivu katika
Kitongoji cha Beni. Askari wengine wanne hawajulikani waliko.
Alisema mbali na kupigwa na roketi hilo, pia
kulikuwa na mashambulizi ya risasi. Hata hivyo, haikufahamika mara moja
askari wangapi wamejeruhiwa na msako mkali unaendelea.


Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, msemaji wa JWTZ,
Joseph Masanja alisema: “Hizo habari ndiyo nimezisikia, ngoja nizifanyie
kazi... siwezi kusema au kukupa habari nusu, tunataka tujue ilikuwaje,
ilitokea nini, kivipi ndipo tutasema.”
Habari zilizopatikana baadaye jana, zilidai kuwa
kutokana na mashambulizi hayo kuwa mazito, raia wa eneo hilo
wamekimbilia porini na wengine kuomba hifadhi kutokana na wasiwasi wa
mashambulizi hayo yaliyotokea umbali wa kilomita sita kutoka Mji wa
Oicha kuendelea.
Mashambulizi hayo yalifanyika wakati askari hao
wakiwa katika doria ya kawaida usiku na inaelezwa kuwa ni kulipiza
kisasi baada ya askari 16 wa Kundi la Allied Democratic Forces (ADF),
kuuawa katika mashambulizi makali mwishoni mwa wiki.
Kikosi hicho cha Tanzania kinachounda Jeshi la
Umoja wa Mataifa, kinashirikiana Jeshi la Serikali la FRDC kukabiliana
na waasi hao wanaodaiwa kutoka Uganda wanaounda Kundi hilo la ADF ambalo
linaendesha vitendo vya uasi, mauaji na utekaji nyara Kaskazini
Mashariki mwa DRC.
Hata hivyo, baada ya mashambulizi hayo, askari wa
FRDC kwa kushirikiana na baadhi wa Tanzania, walianza kufanya msako
mkali kuwakamata waliohusika.
Mkuu wa Misheni ya Monusco, Martin Kobler alisema
jana kuwa wamechukizwa na mashambulizi ya mara kwa mara yanayotokea na
hasa mauaji ya askari wa kulinda amani na raia.
“Ninalaani mashambulizi kwa askari wa Tanzania
waliokuwa na kazi ya kulinda amani kwa raia wa Beni. Natuma salamu zangu
za rambirambi kwa familia za wapiganaji hawa, majeruhi wapone haraka,”
alisema Kobler.
No comments:
Post a Comment