NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba,
amesema kuwa akishindwa katika mchakato wa kura za maoni za kusaka urais
ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), atarudi jimboni kuendelea
kuwatumikia wapiga kura wake.
Kutokana na hali hiyo January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli, amewataka
wananchi wake kuwapuuza watu wanaopita na kudai kuwa wanataka ubunge kwa
kuwa yeye anatajwa katika kinyang’anyoro cha urais ndani ya CCM.
Kauli hiyo aliitoa juzi jimboni kwake Bumbuli, wilayani Lushoto mkoani
Tanga katika mkutano wa hadhara ambapo alikuwa akizungumzia mafanikio na
changamoto za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi tangu alipochaguliwa
mwaka 2010.
January alitumia mkutano huo kuwashukuru wapiga kura wake kwa kumchagua
kuwa mbunge mwaka 2010 huku akisema kuwa kama si wao asingeweza kutajwa
katika mbio za urais ndani ya CCM.
“kutajwa si dhambi na kwa kuwa fomu za uchaguzi si sumu si dhambi kuchukua…. na kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
“Hivi kuna kiu kubwa ya uongozi wa aina mpya na kuna watu wamemwona mtu
na kumtaja yeye jambo ambalo si baya. Wapuuzeni watu wanaopita na kusema
mimi sitaki ubunge eti kwa sababu natajwa kwenye urais.
“Hayo ni maneno ya kilaghai na ya kukatisha tamaa na kichochezi
msiyakubali. Kinyang’anyiro ni kama mchezo wa mpira kuna kushinda na
kushindwa.
“Tukishindwa narudi hapa tuendeleze tuliyoyaanza, Rais Kikwete alijaribu
mara ya kwanza kura hazikutimia akarudi jimboni hata pia Kigoda (Dk.
Abdallah) naye alifanya hivyo ikashindikana akarudi kwenye ubunge,”
alisema.
Akizungumzia hatua ya kufufua uzalishaji wa Kiwanda cha Chai Mponde,
January alisema kuwa Serikali imeridhia kutoa Sh bilioni 4 ambazo ni
gharama za kulipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi.
Alisema mbali na hilo madeni ya malipo ya wakulima, gharama za ukarabati
na mtaji wa kuanzia kuendesha shughuli za uzalishaji utaimarishwa.
January ambaye yupo katika ziara ya siku tano ya kutembelea jimbo lake,
alisema Serikali ilituma wataalamu kufanya tathmini yenye lengo la
kutambua gharama za ufufuaji wa kiwanda hicho kilichokuwa kikiendeshwa
na Chama cha Wakulima wa Chai cha Usambara (Utega) na mwekezaji ambaye
ni Lushoto Tea Company katika miaka ya mwanzo ya 2000.
Alisema kwa kuwa fedha hizo hazikuwa katika bajeti ya Serikali, ilibidi
ofisi ya waziri mkuu kuomba kibali kutoka kwa rais ili kutoa fedha hizo.
“Mambo yote yako tayari. Kilichokuwa kinasubiriwa ni kibali ambacho
kimekwisha kutolewa na Rais Kikwete. Hivi sasa ni Hazina ndiyo
inayosubiriwa itoe fedha hizo kwa ajili ya kukarabati kiwanda na gharama
nyingine,” alisema January.
Mgogoro huo ambao umeleta maumivu makali ya kiuchumi na kijamii kwa
wakulima wapatao 4,000 walioko katika skimu tano za chai zilizopo katika
eneo la Halmashauri ya Bumbuli, ulitatuliwa na Serikali na maamuzi hayo
kutangazwa kwa wakulima na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Abdulrahman Kinana.
Baada ya tamko hilo ambalo amelieleza kuwa la kihistoria la kuchukua
kiwanda kutoka kwa mwekezaji kukirejesha kwa wakulima, January alieleza
kuwa Serikali ilianza harakati za kufufua kiwanda kwa kutuma timu ya
wataalamu kufanya tathmini.
Wazee wambariki
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, wazee wa Bumbuli, walimpa baraka
huku wakimuhakikishia kumwunga mkono katika harakati zake za kisiasa
ndani ya Chama Cha Mapinduzi.
Waliotoa baraka hizo kwa niaba ya wazee ni Askofu Mstaafu wa Kanisa
la Kiinjili na Kirutheli Tanzania (KKKT) Lushoto, Amasia Mweta na Sheikh
Yahya Mjata.
Ni dhahiri mpambano wa kuwania urais ndani ya CCM unazidi kunoga, ikiwa
imebakia miezi michache kabla ya kupulizwa rasmi kipenga.
January Makamba ni mmoja wa makada kutoka CCM waliotangaza nia ya
kuwania urais ndani ya CCM ambaye hivi karibuni aliandika kitabu
kinachoeleza nia yake hiyo.
Katika kitabu hicho pamoja na mambo mengine kinaeleza mikakati ya
mwanasiasa huyo kijana iwapo atapitishwa na chama chake ili kuwania na
hatimaye kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi kitaifa.
Katika kitabu hicho chenye kurasa 196, January anasema rais ajaye lazima
awe na tafakuri pana na nia ya kuendeleza nchi na si kuwa na kaulimbiu
nyepesi za afya bure, elimu bure zisizo na ufafanuzi ili kuwahadaa
wananchi.
Kitabu hicho kilichoandikwa na mchambuzi na mwandishi wa makala za
siasa, Padri Privatus Karugendo kimebeba sera na mikakati yake kiundani
ya kuiongoza nchi iwapo atapatiwa dhamana na CCM kugombea urais.
Katika kitabu hicho kinachoitwa, ‘Maswali na Majibu 40: Mazungumzo na
January Makamba kuhusu Tanzania Mpya’, mwanasiasa huyo anasema uongozi
hauishii kwa kauli za juu juu za kuongeza ajira, kuboresha elimu kwani
kila mtu anaweza kuyasema hayo.
January, anasema katika tafakuri zake anaona rais ajaye anatakiwa
kuzitambua kwa kina changamoto za nchi yake na kuwa na mikakati ya
kuzitatua.
Kutokana na changamoto hizo, Janury anasema ni za kiuongozi na utatuzi
wake unategemea kiongozi mwenyewe, hulka, mtazamo wake na usahihi wa
uamuzi anaoufanya.
“Kuomba uongozi wa nchi si harakati binafsi na wafuasi wako kupata vyeo.
Ni dhamana kubwa ya kujenga mustakabali wa nchi na kuwaunganisha
Watanzania wote. Kwa hiyo, uamuzi wa kugombea lazima uupe heshima na
nafasi inayolingana na dhamana yenyewe,” anasema January katika kitabu
hicho.
No comments:
Post a Comment