Wakati wateja wa umeme wamendelea kutaabika, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limetoa malekezo zaidi ya namna ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi.
Taarifa ya Tanesco imekuja baada ya tatizo
lililojitokeza kwa baadhi ya mawakala wa Luku kushindwa kutoa huduma ya
kuuza umeme na kusema litamalizika karibuni.
Hali hiyo imetokana na Kampuni ya Selcom ambaye ni
wakala wa kuuza na kuziunganisha baadhi ya kampuni za simu kwa Tanesco
kusitishiwa huduma kutokana na kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza
baadhi ya majukumu yake ikiwamo kughushi nyaraka na kukiuka taratibu za
kulipa kodi.
Taarifa iliyotolewa jana na shirika hilo, na
kusainiwa na Ofisa Habari wake, Adrian Sevelin ilisema kuwa huduma
zinaendelea kupatikana kupitia Kampuni ya MAXCOM katika Vituo
mbalimbali, ATM za CRDB na NMB, NMB Mobile pamoja na ofisi zote za
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) nchi nzima hadi siku ya Jumamosi na
Jumapili na siku za Sikukukuu kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 2:00
usiku.
“Shirika linaomba radhi kwa usumbufu wowote
unaojitokeza, wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila kitu
kinakwenda sawa”alisema Sevelin.
Wakazi wa Dar waonja joto ya jiwe
Gazeti hili lilizunguka katika vituo mbalimbali
vya kutoa huduma hiyo na kukuta misululu ya wananchi wakisubiri huduma
hiyo huku kukiwa na tatizo la mtandao.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati
tofauti katika vituo mbalimbali kikiwamo cha Kisutu, Kinondoni Mkwajuni,
Buguruni Sheli, Gongo la Mboto, Faya, Mwananyamala , Mwenge Mpakani,
Kigogo, Tandale, Mbagala Zakhem, walisema kuwa wamesimama katika foleni
hizo kusubiri huduma hiyo tangu saa 12 asubuhi.
Imelda Wahuzi aliyekutwa katika kituo cha Buguruni
alisema kuwa ameanza kupata adha hiyo tangu jana mchana , ambapo
aliahirisha kununua akiadhimia kudamka asubuhi ya leo, lakini anashangaa
amefika kituoni hapo saa 12asubuhi na hadi saa nne asubuhi hajapata
umeme.
Muuza umeme katika kituo hicho ambaye alikataa
kutaja jina lake alisema kuwa pamoja na watu kuja kwa wingi kupata
huduma hiyo katika kituo hicho bado kuna tatizo la mtandao kusumbua
ndiyo maana foleni inakuwa kubwa.
Alisema kama siyo mtandao kusingekuwa na foleni,
huku akikiri kuwa hajawahi kuwa na watu wengi kama siku hizi mbili,
yaani juzi na jana.
Ibrahimu Hassan aliyekutwa katika foleni Kisutu
alisema kuwa amelazimika kusitisha shughuli zake baada ya siku iliyopita
kupata hasara kwa sababu hakufanya kazi katika kiwanda chake cha
kuchomelea mageti kutokana na kukosa umeme.
No comments:
Post a Comment