Real Madrid wameduwazwa na Juventus baada ya Carlos Tevez na mchezaji wao wa zamani, Alvaro Morata kufumania nyavu zao kwenye mechi waliyopigwa 2-1.
Wakicheza mjini Turin, Real Madrid waliendeleza unyonge kwa timu za Italia kwenye ardhi yao, kwani katika safari zao nane huko hawakuweza kushinda.
Ilikuwa ni katika mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) Jumanne hii, ambapo Juventus wanajaribu kufika fainali kwa mara ya kwanza tangu 2003.
Cristiano Ronaldo aliwafungia mabingwa hao wa Ulaya bao lake la 54 kwa msimu huu kwenye mashindano yote, huku akimzidi Lionel Messi wa Barcelona kwa bao moja kwenye UCL, kwani anayo 76 wakati Messi anayo 75.
Carlo Ancelotti,
kocha wa Real atatakiwa kusuka mipango upya ili walau wapate ushindi wa
bao 1-0 nyumbani Mei 13, ambao utatosha kuwafikisha fainali watetee
taji lao.
Morata alifunga bao baada ya kipa wa Real, Ike
Casillas kuutema mpira wa Tevez. Ronaldo alisawazisha baada ya kunasa
majalo ya James Rodriguez.
Real waliteleaz tena kipindi
cha pili, ambapo Tevez akienda kufunga alikwatuliwa na Dani Carvajal,
Juve wakapewa penati iliyotiwa kimiani vyema na Tevez.
Kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri
alionekana kuridhishwa na mabao hayo, kwani muda mfupi baada ya kuingia
bao la pili, aliongeza beki wa kati, Andrea Bazagli badala ya
mshambuliaji Sturaro na kuwamaliza Real.
Ancelotti
alijaribu kutupa karata nyingine kwa kumwingiza Javier Hernandez
‘Chicharito’ aliyewavusha hatua iliyopita, akimtoa Isco, lakini mambo
yalibakia magumu.
Nahodha wa Juve, kipa Gialuigi Buffon aliongoza wachezaji na washabiki kushangilia kwa nguvu baada ya kipenga cha mwisho.
Hata hivyo, ikiwa tofauti hiyo ya bao moja itawasaidia, itajulikana kwenye mechi ya marudiano itakayopigwa Santiago Bernabeu.
Juventus
waliweka rekodi UCL kwenye mechi hiyo, ambapo kabla ya Morata kufunga
bao, walipigiana pasi 27 ambazo hazijapata kutokea msimu huu, Real
wakionekana kupoteana.
Wataliano hao wamepoteza mechi moja
tu kati ya 18 za mashindano ya Ulaya kwenye uwanja wao na ushindi dhidi
ya Real umekuja siku chache baada ya kuutwaa ubingwa wa Italia kwa mara
ya nne mfululizo.
Kufungwa huku kunamuweka Ancelotti wa Madrid katika hali ngumu, ambapo tayari kuna tetesi za kwamba huenda akafutwa kazi mwisho wa msimu
No comments:
Post a Comment