TIMU ya Simba imerudisha matumaini ya kushiriki michuano ya kimataifa
mwakani baada ya kuwachapa wapinzani wao, Azam FC mabao 2-1 mchezo
uliofanyika jana Uwanja wa Taifa jijini hapa.
Simba na Azam zipo kwenye vita kali ya kuwania nafasi ya pili ili
kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani, ambapo wekundu hao
wameshindwa kukata tiketi ya michuano ya kimataifa toka mwaka juzi
waliposhiriki mara ya mwisho.
Azam ambayo mara baada ya mchezo huo imebakiwa na pointi 45 ikiwa na
mechi mbili mkononi dhidi ya Yanga keshokutwa na Mgambo JKT Jumamosi
hii, inahitaji pointi tatu tu kwenye mechi hizo zitakazoifanya kufikisha
pointi 48 ambazo hazitaweza kufikiwa na Simba.
Simba yenye pointi 44 inabidi iiombee mabaya Azam ipate sare mechi
hizo au ifungwe zote, huku na yenyewe ikitakiwa kuifunga JKT Ruvu kwenye
mchezo wa mwisho Jumamosi hii ili kupata tiketi ya michuano hiyo.
Wekundu hao walianza kwa kasi mchezo huo na kufanya kosakosa langoni
mwa Azam kupitia kiungo, Said Ndemla dakika ya 12 aliyepiga shuti kali
la mbali ambalo lilidakwa vema na kipa Aishi Manula.
Azam waliamka dakika ya 14 na kufanya shambulizi kali langoni mwa
Simba kupitia kwa Kipre Tchetche, lakini Didier Kavumbagu anakosa bao la
wazi akiwa na kipa Ivo Mapunda, baada ya kupiga shuti hafifu
lililodakwa kirahisi.
Dakika ya 37, mwamuzi wa kati, Israel Nkongo wa jijini hapa alimuonya
kwa kadi ya njano kiungo wa Azam, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa
kumchezea madhambi kiungo wa Simba, Jonas Mkude.
Azam ilipata pigo dakika mbili baadaye baada ya Sure Boy kupewa kadi
nyekundu ya moja kwa moja kwa kumfanyia madhambi beki Mohamed Hussein na
hivyo kulazimika kucheza pungufu hadi mwisho wa mchezo.
Kabla ya timu zote kwenda mapumziko, ilitokea piga nikupige langoni
mwa Simba baada ya kiungo wa Azam, Frank Domayo kuingiza krosi
iliyowababatiza mabeki wa Simba na Mapunda alilazimika kufanya kazi ya
ziada kuokoa na kufanya kipindi cha kwanza kuisha kwa suluhu.
Azam ilifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kumtoa Domayo na
kuingia Bryson Rafael, kisha ikamtoa beki Pascal Serge Wawa na kuingia
kiungo Mudathir Yahya.
Simba ilitumia vema mwanya wa Azam kuwa pungufu kwa kupata bao la
uongozi dakika ya 48 lililofungwa na mshambuliaji Ibrahim Ajibu
akiunganisha vema pasi ya beki Hassan Kessy.
Dakika ya 53, Azam ilijibu mapigo kwa kusawazisha kupitia kwa
Mudathir aliyeingia kipindi cha pili, kiungo huyo alipokea pasi ya
Tchetche na kupiga shuti akiwa ndani ya eneo la 18 lililomshinda kipa wa
Simba.
Azam iliyovuliwa ubingwa wa ligi na mabingwa wapya Yanga Jumatatu
iliyopita, ilifanya mabadiliko dakika ya 67 kwa kutoka Kavumbagu na
kuingia nahodha John Bocco aliyetoka kwenye majeruhi.
Simba ilimaliza mchezo huo dakika ya 74 kwa kupata bao la pili
lililofungwa na Ramadhan Singano ‘Messi’ baada ya kupiga krosi
iliyodunda chini na kutinga wavuni moja kwa moja, Messi alifunga
akitumia vema pande la Mkude.
Mwamuzi alilazimika kumwonyesha kadi ya njano Messi baada ya
kushangilia bao hilo kwa kuvua jezi yake. Licha ya dakika saba kuongezwa
kufuatia dakika 90 kumalizika, Simba ilimaliza mpira huo kwa ushindi
huo.
Oscar Assenga kutoka Uwanja wa Mkwakwani, Tanga naye anaripoti kuwa,
wenyeji Coastal Union wamefanikiwa kujiondoa kwenye janga la kushuka
daraja baada ya kuichapa Stand United mabao 3-1 na kufikisha pointi 31.
Mabao ya Coastal yaliyoiweka kwenye hali mbaya Stand yamefungwa na
Ayoub Semtawa dakika ya 17, Yusuph Chuma (dk 42) na Mnigeria, Bright
Obina (dk 69), huku lile la Stand likifungwa na Mnigeria, Chidiebere
Abisirim.
No comments:
Post a Comment