Tuesday, 5 May 2015

WALIOKUMBWA NA MAAFURIKO WAOMBA MSAADA ...>>

Wananchi wa Kata ya Arusha chini, Wilaya ya Moshi wamewaomba viongozi wa Serikali kuwapatia msaada wa chakula na mavazi kutokana na  vitu vyao kusombwa na maji ya mvua inayoendelea kunyesha.
 
Wananchi hao ni wa vijiji saba katika wilaya hiyo ambavyo vimezingirwa na maji kutokana na mafuriko mkoani Kilimanjaro.
Walisema hayo jana wakati wakipokea msaada wa vyakula, sabuni  na madaftari kutoka kwa mmoja wa wadau wa maendeleo ya Moshi Vijijini ambaye pia ni kada wa Chadema, Clemence Chuwa.
Mmmoja wa wananchi hao Elina Motere alisema, katika maeneo hayo hakujawahi kutokea mafuriko makubwa kiasi hicho na kwamba chakula na mavazi vimesombwa na wao kubaki wakiwa hawana kitu.

 
“Sisi tumebaki kama tulivyo, vyombo vyote pamoja na magodoro, vimesombwa na maji tunahitaji msaada wa hali na mali ili tuweze kuishi,” alisema Motere.
Alisema viongozi wa Serikali wamekuwapo katika eneo hilo lakini hawana msaada wa kutosha kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Bakari Mussa alisema pamoja na msada wanaopewa bado hali zao ni mbaya kwa kuwa wanahitaji vitu vingi.
Hata hivyo, alitoa shukrani zake kwa msaada huo na kuiomba Serikali kuwapelekea haraka chakula pamoja na mavazi.
Kwa upande wake Chuwa amewataka wadau  mbalimbali hususani wa Moshi Vijijini kuwasaidia wananchi hao ili waweze kujikimu kimaisha.
“Nimeguswa, kuwasaidia wananchi hao ni sawa na ndugu zangu kutoa ni moyo nawaomba wadau wengine wajitokeze kuwasaidia  kwa kuwa hawana chakula wala mavazi,” alisema Chuwa.
Alisema ametoa msaada wenye thamani ya Sh500,000 kwa kuwanunulia  mchele, unga, sabuni, mafuta ya kupikia, madaftari, pamoja na kalamu ili kuwasaidia wanafunzi  wa kata hiyo.
Vijiji vilivyoathirika ni pamoja na Uwanja wa Ndege, Kati, Langasani Magharibi na Mashariki, Makumbusho na River Side.

No comments:

Post a Comment