Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikieleza
kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kuwa uchaguzi huo unaweza
kuahirishwa kama ilivyotokea kwenye Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa.
Kikatiba, uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na
madiwani unatakiwa kufanyika Jumapili ya mwisho ya Oktoba ambayo itakuwa
Oktoba 25, mwaka huu ikiwa ni mwaka wa tano tangu kuchaguliwa kwa
Serikali iliyopo madarakani.
Katika kipindi hicho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) ilitakiwa kurekebisha mara mbili Daftari la Kudumu la Wapigakura
lakini haijafanya hivyo hata mara moja na hii ya sasa inayoendelea
katika baadhi ya mikoa bado inasuasua.
Kutokana na kusuasua huko, NEC ililazimika kuahirisha Kura ya Maoni iliyokuwa imepangwa kufanyika Aprili 30, hadi tarehe itakayotangazwa baadaye, licha ya awali kuelezwa mara kwa mara na tume yenyewe au viongozi wa Serikali kuwa kura hiyo ilikuwa palepale.
Ni kutokana na hali hiyo, Chadema na vyama
washirika vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vilieleza
wasiwasi wa kuwapo uwezekano wa kuahirisha uchaguzi mkuu kwa kisingizio
cha kutokamilika uandikishaji wapigakura kama ilivyofanyika kwa kura ya
maoni.
Lakini akihutubia siku ya wafanyakazi (Mei Mosi),
mjini Mwanza, Rais Kikwete alieleza kuwashangaa wapinzani hao, akisema
ni aibu kwao kuzua jambo ambalo halipo, kwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba
uko palepale na hana mpango wa kuongeza muda.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva
jana alisisitiza kauli ya Rais akisema uchaguzi huo utafanyika kama
Katiba inavyoeleza (wiki ya mwisho ya Oktoba), huku Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama akisema
uandikishaji unavyoendelea ni kielelezo kwamba uchaguzi utafanyika kama
ulivyopangwa.
Wasiwasi wa Mbowe
Akifungua kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu
jana, Mbowe alisema: “Wote hatujui kama uchaguzi mkuu upo mwaka huu,
waziri mkuu anasema upo, NEC wanasema upo lakini mazingira hayaonyeshi
kwamba utakuwapo mwaka huu.”
Alisema bado uandikishaji wapigakura unasuasua na
mazingira hayaonyeshi kwamba utakamilika kabla ya siku ya uchaguzi
inayoelekezwa na Katiba.
Alisema hata kwenye kura za maoni ya Katiba
Inayopendekezwa, mazingira yalionyesha kwamba isingewezekana ifanyike
Aprili 30, mwaka huu kama Serikali ilivyotangaza.
No comments:
Post a Comment