Mzunguko wa 37 wa Ligi Kuu ya England (EPL) umetoa matokeo mchanganyiko yanayoathiri timu za mkiani na zinazotafuta walau nafasi ya nne.
Wakati Liverpool wamecharazwa 3-1 na Crystal Palace wakiwa katika siku ya kumuaga nahodha wao Steven Gerrard nyumbani, Hull wamepoteza mechi muhimu na sasa wapo katika hali mbaya.
Southampton nao wamekuja kwa mtindo wa aina yake, wakiwakandika Aston Villa 6-1, huku mchezaji wao, Saido Mane akiweka rekodi ya kufunga mabao matatu katika muda mfupi zaidi tangu kuanzishwa kwa EPL.
Hull wakiwa ugenini wameshinda kuhimili vishindo vya Tottenham Hotspur na kukubali kuchapwa 2-0 hivyo kuweka rehani nafasi yao EPL, wakitakiwa washinde mechi yao ya mwisho dhidi ya Manchester United wikiendi ijayo.
Hull au Tigers kama wanavyojiita wapo pointi mbili tu juu ya mstari wa hatari na katika mechi ya Jumamosi hii walifungwa kwa mabao ya Nacer Chadli na beki wa pembeni, Danny Rose.
Ili wabaki EPL, watahitaji Newcastle washindwe kuwafunga West Ham kwenye mechi ya mwisho au Sunderland wapoteze kwa mechi yao dhidi ya Arsenal na nyingine kwa Chelsea na wao wawafunge United.
Katika mechi nyingine, Liverpool walionesha kwamba hawawezi tena kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) walipokubali kichapo kutoka kwa Palace, kwani kwa mechi moja waliyobakiza, wakiwa na pointi 62 hawawezi kuwafikia walio nafasi ya nne, Manchester United wenye pointi 68.
Kadhalika walishindwa kutoa heshima kwa nahodha wao Gerrard na sasa watatarajia kuingia kwenye Ligi ya Europa kama hawatazidiwa nguvu na Southampton na Swansea katika mechi za mwisho.
Washabiki wa Liverpool walimiminika kwa wingi kwa ajili ya kumuaga nahodha wao, Palace wakakaa kimya, na Liver wakafurahi Adam Lalana alivyotangulia kuwapa bao.
Hata hivyo, vijana wa Alan pardew walisawazisha kupitia kwa Jason Puncheon kabla ya Wilfried Zaha na Glenn Murray kupigilia misumari ya mwisho.
Southampton waliwakung’uta bila huruma Astona Villa 6-0, ambapo Saido Mane aliweka rekodi ya kufunga mabao matatu ndani ya dakika mbili na sekunde 56 ambayo haijapata kuwekwa tangu kuanza kwa EPL.
Burnley ambao tayari wameshuka daraja walikwenda suluhu na Stoke, QPR wakawafunga Newcastle 2-1 wakiwa wanakumbuka shuka wakati kunakucha, lakini ukiwa ni ushindi wa kwanza dhidi ya Magpies tangu 1995.
QPR tayari wameshuka daraja lakini walicheza kulinda heshima yao na matokeo yake ni kwamba Newcastle wanaweza kushuka daraja kutegemeana na matokeo ya mechi yao ya mwisho dhidi ya West Ham, ambapo ili kujihakikishia wanabaki EPL watatakiwa kushinda.
West Ham wenyewe walifungwa na Everton 2-1 katika mechi ambayo matokeo yake hayabadili sana mambo, kwa sababu hizi ni aina ya klabu ambazo hazitarajii kushuka daraja wala kupata nafasi za kucheza michuano ya Ulaya.
Jumapili hii Swansea wanawakaribisha Manchester City na Manchester United watakuwa wenyeji wa Arsenal katika mechi zinazoweza kuweka msingi wa nani atakuwa nafasi ya pili, tatu na nne.
Jumatatu itakuwa zamu ya Chelsea na West Bromwich Albion kwenye mchezo ambao ni wa kuendelea kukamilisha ratiba tu na kutunza heshima.
Jumatano Arsenal na Sunderland watamaliza mechi ya kiporo chao cha mchezo mmoja kwa kumenyana kwenye dimba la Emirates ili wawe sawa na wengine, tayari kwa kipite cha mwisho Jumapili inayofuata ili kufunga pazia la EPL.
Msimamo ulivyo kwa sasa ni Chelsea ambao ni mabingwa kuwa na pointi 84, Manchester City 73, Arsenal 70, Man United 68, Liverpool 62, Spurs 61, Southampton 60 na Swansea 56.
Katika hatari ya kushuka daraja ni Aston Villa wenye pointi 38, Sunderland pointi 37, Newcastle 36 na Hull walioambulia 34.
Waliokwishashuka tayari na ambao wamebakisha mechi moja za kukamilisha ratiba wakijiandaa na safari ya Championships ni Burnley wenye pointi 30 sawa na QPR, bali wanatofautiana na uwiano wa mabao ya kufungwa na kufungwa, Burnley wakiwa na -26 na QPR wakiwa na -27.
No comments:
Post a Comment