Sunday, 17 May 2015

KUFA KUFAANA ... FUSO LAPINDUKA MASELA WALAMBA GAMBE MWA MWI !!! >>>

 

Baadhi ya watu jana ‘waligida’ pombe za bure baada ya Fuso lililokuwa limebeba masanduku ya bia kupinduka katika Barabara ya Mandela, Dar es Salaam.
Tukio hilo limetokea mchana eneo la Tabata TIOT, baada ya gari hilo kugongwa kwa nyuma na lori na kupinduka.

Kutokana na ajali hiyo, kundi la vijana lilivamia na kuchukua chupa za bia huku wengine wakinywa mfululizo.

Mwandishi wa gazeti hili aliyekuwa eneo la tukio alishuhudia vijana hao wakiwamo madereva wa bodaboda, wa magari makubwa na wapita njia wakiokota chupa za bia hizo na kunywa.

Tukio hilo la aina yake, lilidumu kwa takribani 20 kabla ya polisi kuongeza nguvu kutoka askari wawili waliokuwa eneo hilo wakizuia watu kuchukua chupa.

Vijana walionekana kuhatarisha usalama wao kwa kuingia mitaroni ambako bia zilingukia humo na kuzichukua bila kujali kuwa zimepasuka.

Vijana wengine walionekana kuanza kulewa kwa kunywa bila kipimo.

Dereva wa Fuso hilo, kutoka Kampuni ya Mwanahela, Mohamed Said alisema mzigo huo wa bia aliutoa katika Kiwanda cha Serengeti kwenda Kituo cha Polisi Mkoa wa Pwani.

“Hizi bia zilikuwa katika masanduku 500, ni mali ya Polisi Pwani, ajali hii ni uzembe unaoonekana wazi kuwa wa dereva wa lori, hata polisi wakija kupima watajua nani mwenye kosa,” alisema Said kabla ya Fuso lingine kufika na kuchukua bia hizo na kuondoka nazo.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori aliyekuwa akitokea njia ya pembeni kuingia barabara kuu bila tahadhari.

Hata hivyo, Dereva wa lori hilo, Godfrey Baregu alisema kosa lilisababishwa na uzembe wa dereva wa Fuso ambaye alitakiwa kusubiri ili yeye (Baregu) apite.

No comments:

Post a Comment