Sunday, 17 May 2015

UZALISHAJI WA SUKARI WAZIDI KUPOROMOKA ...>>

Wadau wa viwanda vya sukari nchini wameitupia Serikali lawama kwa kushindwa kuisimamia sekta hiyo na kusababisha uzalishaji kushuka kwa asilimia 20 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. 
                              
Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa wadau hao, uliofanyifa Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Chama cha Wazalisha Sukari nchini, Deo Lyatto alisema miaka ya nyuma wadau hao walijivunia ardhi, maji, masoko na nguvu kazi zilizokuwapo kwa wingi, lakini sasa kuna matatizo lukuki.

“Sasa tunachojivunia pekee ni uvumulivu tu,” alisema Lyatto na kuongeza kuwa uingizaji wa sukari nyingi nchini umeharibu uimara wa soko la bidhaa hiyo.

Alisema hakuna tozo maalumu inayotozwa na Serikali kwa sukari inayoingizwa ili kuokoa wafanyabiashara wazawa.

Lyatto alisema kutokana na kutokuchukuliwa kwa hatua, wakulima wa miwa wamepunguza uzalishaji kutoka tani 300,000 hadi tani 60,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 15.

Hata hivyo, Lyatto alisema Serikali ipo katika mchakato wa kutunga sheria zitakazosaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Henry Semwanza alisema wakulima wadogo wa miwa wamelima kwa wingi zao hilo, lakini viwanda vinashindwa kununua, hivyo kukiuka malengo ya kubinafsishwa kwa viwanda hivyo.

“Wakati vinabinafsishwa tuliambiwa ifikapo mwaka 2011 hakutakuwa na upungufu wa sukari, lakini bado tatizo lipo, njia ya kuondokana na tatizo hili ni kuanzisha viwanda vidogo na vya kati vitakavyokuwa vikinunua miwa kwa wakulima,” alisema Semwanza.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Winfred Kaliwa alisema Serikali imefanya jitihada za kutosha kuongeza uzalishaji wa miwa na kwamba iwapo kuna watu wanamapendekezo ya kuboresha zaidi wawasilishe katika ofisi husika.

No comments:

Post a Comment