Thursday, 14 May 2015

Milio ya risasi na milipuko ya mabomu vimesikika usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi wiki hii mjini Bujumbura, nchini Burundi.

Mpaka sasa haijajulikana kundi gani lina mamlaka ya uongozi wa nchi, baada ya kundi la wanajeshi linaloongozwa na jenerali Godefroid Niyombare kutangaza kuipindua serikali ya Pierre Nkurunziza.

Jenerali Godefroid Niyombare akiwasili kwenye kituo cha redio RPA, Alhamisi Mei 13 jioni.
REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana
Jumatano wiki hii, mkuu huyo wa zamani wa majeshi, ambaye pia aliwahi kuwa mkuu Idara ya ujasusi kwa kipindi cha miezi mitatu, alitoa tangazo la kuipindua serikali ya Nkurunziza wakati rais huyo alikua alijielekeza jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania, kushirika mkutano wa marais wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu mgogoro unaoendelea kushudiwa nchini Burundi.
Kwa muda wa wiki 3 Burundi imekua ikishuhudia maandamano ya raia wakipinga muhula wa tatu wa Pierre Nkurunziza. Kwa muda wa majuma kadhaa mitandao ya kijamii imekua imefungwa, lakini baada ya jaribio hilo mapinduzi mitandao hiyo imefunguliwa.
Kituo cha redio RPA ambacho kimekua kimefungwa tangu maandamano hayo yaanze, kimeanza kupeperusha matangazo yake baada ya jaribio hilo mapinduzi, hata redio za kibinafsi mbili ambazo ni Bonesha Fm na Isanganiro, ambazo matangazo yake yalikua hayasikiki mikoani na katika baadhi ya maeneo ya nchi jirani, kwa sasa matangazo ya redio hizo yanasikika.
Mapema Jumatano asubuhi, raia kutoka wilaya zote za mji wa Bujumbura walikua wakijaribu kuingia mjini kati Bujumbura, bila mafaanikio. Lakini kuna kundi la wanawake na wasichana ambao walifaulu kuingia kwenye eneo la Uhuru mjini Kati Bujumbura.
Hata hivyo Ikulu ya rais imeendelea kutangaza kupitia akaunti yake ya twitter kuwa mapinduzi hayo yamefeli, baada ya jeshi kuingilia kati na kudhibiti hali ya mambo. Hata hivyo raia waliingia kwa wingi mjini kati Bujumbura baada ya kusikia tangazo hilo la jeshi la mapinduzi ya serikali, huku askari polisi wakionekana kuingia katika makambi yao.
Wakati huo huo wanajeshi wengi wameonekana wakiizingira redio na televisheni vya taifa pamoja na uwanja wa ndege wa Bujumbura.
Mpaka asubuhi saa moja (saa za Afrika ya Kati) milio ya risasi na milipuko ya mabomu imeendelea kusikika

No comments:

Post a Comment