Monday, 18 May 2015

NKURUNZINZA AONEKANA HADHARANI KWA MARA YA KWANZA ...>>>

                                        Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza aonekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza Jumapili mwishoni mwa juma hili lililopita tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi Jumatano Mei 13 mwaka 2015.

Kuonekana hadharani kwa Pierre Nkurunziza kumesitisha uvumi kwamba rais huyo hajarejea nchini Burundi.

Pierre Nkurunziza amewapokea wanahabari nyumbani kwake na kusema kwamba Burundi inakabiliwa na vitisho vya wanamgambo wa kiislamu wa Kisomalia wa Al Shabab.
" Tuko hapa kuwaambia kwamba tunapaswa kuwa makini na tishio la Al Shabab na tutachukua hatua muhimu za kukabiliana na mashambulizi ya wanamgambo wa kundi la Al Shebab", amesema rais Pierre Nkurunziza.

Kundi la Al Shabab kupitia msemaji wake amekanusha madai hayo ya rais Nkurunziza ya kushambulia nchi yake. Al Shabab imesema huo ni mpango wa Pierre Nkurunziza na serikali yake wa kutaka kuwakandamiza waandamanaji ili wasiendelei kuandamana dhidi ya muhula wake wa tatu.

Awali rais Pierre Nkurunziza hakupendelea kuzungumza na wanahabari, lakini imeonekana kuwa alishinikizwa na washirika wake wa karibu ili aweze kuondoa uvumi uliyokua ukizagaa tangu Ijumaa juma lililopita kwamba rais huyo hayupo nchini Burundi, na huenda picha na sauti yake viliyorushwa hewani kwenye redio na runinga vya taifa vilirikodiwa nje ya nchi alipokua, baada jaribio la mapinduzi.

Hata hivyo rais huyo hakueleza kuhusu jaribio la mapinduzi na kupingwa kwa muhula wake wa watatu. Wakati huo huo mshauri wake mkuu anayeshusika na masuala ya mawasiliano Willy Nyamitwe, ameeleza kwamba kuna uwezekano wa kuahirisha kwa wiki kadhaa uchaguzi wa madiwani na wa wabunge uliyopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Mei.

Hayo yakijiri, vyama vya kiraia pamoja na vyama vya kisiasa vya upinzani ikiwa ni pamoja na baadhi ya wafuasi wa chama tawala cha Cndd-Fdd wamesema wataendelea na maandamano Jumatatu wiki hii, wakibaini kwamba jaribio la mapinduzi lilioendeshwa Jumatano wiki iliyopita lilikua ni mpango wa serikali wa kutaka kuzima maandamano, vyama vya kiraia pamoja na kusitisha matangazo ya vituo vya redio na televisheni vya kibinafsi.

Itafahamika kwamba vituo vine vya redio za kibinafsi ikiwa ni pamoja na redio Isanganiro, Bonesha Fm, RPA na redio na televisheni Rennaissance Fm, vilishambuliwa kwa roketi. Polisi inanyooshewa kidole kuhusika na mashambulizi hayo.

No comments:

Post a Comment