Uchunguzi umebaini kuwa kuna viwanja ambavyo havijaendelezwa kwa zaidi ya miaka 20, huku wamiliki wake wakiwa wamerundika mawe, mchanga na kokoto, jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Mipango Miji.
Baadhi ya viwanja hivyo viko katikati ya mji kwenye maeneo ya kibiashara na hakuna dalili ya wamiliki wake kuanza ujenzi kama sheria inavyotaka. Masharti ya uendelezaji wa viwanja kama ilivyo katika Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 1960, inataka ujenzi uwe umekamilika baada ya miezi 36 kuanzia tarehe ya toleo.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael alipoulizwa kuhusiana na tatizo hilo, alisema viwanja hivyo vinapaswa kurudishwa kwa halmashauri.
“Hivyo vilivyopo katikati ya mji kama wameshindwa kuviendeleza ndani ya muda wa kisheria wanatakiwa wavirudishe halmashauri au wanyang’anywe ili wapewe wawekezaji wengine.
“Tunaamini tukikabidhiwa viwanja hivyo tutapata watu wa kutusaidia kuwekeza na watasaidia kukuza uchumi wa Moshi hasa kwa kutoa ajira kwa wananchi wetu hususan vijana,” alisema Meya Michael.
Kuhusu viwanja vya makazi ambavyo havijaendelezwa, Michael alisema hilo ni jukumu la mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kufanya ukaguzi na kuanzisha mchakato wa kuwanyang’anya wamiliki walioshindwa kujenga.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Shaban Ntarambe alisema upo mchakato wa kisheria wa kutwaa maeneo yasiyoendelezwa kwa mujibu wa sheria na kinachotakiwa sasa ni kuyaorodhesha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri hiyo, Ray Mboya alisema kuna viwanja 200 vinavyosubiri baraka za Rais Jakaya Kikwete ili hati zake zifutwe na kuvirudisha Halmashauri.
No comments:
Post a Comment