MWENENDO wa uchunguzi dhidi ya madai ya Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa kutaka kuuawa na
mlinzi wake binafsi, Khalid Kangezi, umezua shaka.
Hii inatokana na ukimya wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam ambapo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa limeshindwa kuwahoji
watuhumiwa waliotajwa na Dk. Slaa.
Gazeti hili limebaini kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula
pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana ambao kwa
pamoja wanashutumiwa kula njama ya kutaka kumzuru Dk. Slaa kwa
kumshirikisha mlinzi binafsi wa kiongozi huyo wa Chadema, hawajahojiwa.
Si hivyo tu, Mchungaji Isack Loyd ambaye Kagenzi anamsukumia kuhusika na
mipango hiyo, naye amesema hajapokea wito wowote wa Jeshi la Polisi
kuhusu kuhojiwa.
Akizungumzia mwenendo wa kesi hiyo, Dk. Slaa aliliambia gazeti hili kuwa
haridhishwi na jinsi Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
linavyoshughulikia kesi hiyo, hivyo alisisitiza kwamba hatokaa kimya
kuzungumzia suala hilo.
Aliongeza kwa kusema kuwa amejaribu kufuatilia kwa karibu mwenendo wa
hatua zinazochukuliwa kuhusu kesi hiyo na kubaini kuwa viongozi wa CCM
ambao wanadaiwa kula njama na mlinzi wake binafsi ili wazuru maisha yake
bado hawajahojiwa.
“Si Mangula wala Kinana na hata huyo bwana Ngowi bado hawajahojiwa na
Jeshi la Polisi na wakati mashahidi wote wameshahojiwa, ushahidi upo
hata namba za mawasiliano ambazo waliwasiliana na mlinzi wangu
tumewakabidhi ofsini kwao…lakini inasikitisha kuona watu walioendesha
njama ya kutaka kuteketeza maisha yangu wanaendelea kuranda randa pasipo
hatua yoyote kuchukuliwa,” alisema Dk. Slaa.
Alisema amejaribu kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa kesi hiyo na mara
kadhaa Polisi wamekuwa wakimwambia kuwa faili la kesi hiyo bado lipo kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
“Ninazo taarifa kuwa viongozi wa CCM wamekaa kikao cha kutaka kuzima
kesi hiyo lakini nimesema sitokaa kimya…nimechoka kuvumilia vitendo vya
namna hii, mwaka 2010 niliwekewa vinasa sauti chini ya kitanda changu
lakini mpaka leo polisi hawajatoa ripoti yoyote ya uchunguzi
waliouahidi,” alisema Dk. Slaa.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Philip Mangula, ili
athibitishe kama ameshahojiwa na Jeshi la Polisi au la, alishindwa
kukataa wala kukubali badala yake alimwambia mwandishi kuwa yupo kwenye
kikao na hata alipotafutwa Kinana simu yake haikupatikana.
Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova ambaye alijibu kuwa hafahamu
chochote hivyo alimtaka mwandishi wa habari hii awasiliane na wasaidizi
wake.
“Ngoja niulize wasaidizi wangu…Lakini kwanini umeniuliza swali hilo
wakati sipo ofisini? Nitafute Jumatatu,” alijibu Kamishna Kova.
Madai ya kutaka kumzuru Dk. Slaa yaliibuka mapema Machi baada ya mlinzi
wake binafsi, Kangezi kutekwa nyara na watu wanaotajwa kuwa ni makada wa
chama hicho na kisha kumtesa kwa saa kadhaa kabla ya kwenda kumshtaki
katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
No comments:
Post a Comment