Tuesday, 28 April 2015

BURUNDI HALI TETE .. JUMUIA ZA KIMATAIFA ZAINGIA WASI WASI ...

  Makabiliano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji Bujumbura, baada ya Pierre Nkurunziza kutangazwa na chama chake kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais.

Nchini Burundi, maandamano yameingia kwa siku ya tatu mfululizo Jumanne wiki hii, siku tatu baada ya mashirika ya kiraia na vyama vya upinzani kuwataka raia kuingia mitaani kupinga rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.

Katika wilaya ya Nyakabiga maandamano yameanza mapema Jumanne asubuhi, huku waandamanaji wakiweka vizuizi kwenye barabara ya Imprimerie na kuchoma moto matairi na miti.

Wakati huo huo Jumuiya ya kimataifa imetoa wito kwa utulivu. Jumuiya ya kimataifa imewataka wanasiasa pamoja na serikali ya Burundi kuheshimu Mkataba wa Arusha uliyoafikiwa mwaka 2000, ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe viliyodumu zaidi ya mwongo mmoja.

Balozi za nchi za Magharibi zimefahamisha kwamba zinafuatilia kwa karibu na kutiwa wasiwasi na vurugu zinazoendelea kushuhudiwa katika mji wa Bujumbura. Umoja wa Ulaya umelaani kukamatwa kwa mwanaharakati wa haki za binadamu Pierre-Claver Mbonimpa na kutoa wito kwa utulivu.
" Sisi tunaendelea kuwatolea wito wanasiasa na serikali ya Burundi kushughulikia suala la uchaguzi katika hali ya maridhiano kwa maslahi ya nchi na kuheshimu makubaliano ya Arusha", amesema Catherine Ray, msemaji wa Umoja wa Ulaya anayehusika na mambo ya nje.

" Tunatiwa wasiwasi na hali inayoendelea kushuhudiwa wakati huu. Katika hatua hii , tunatolea wito serikali kuhakikisha kuwa haki za kiraia na kisiasa zinaheshimishwa, kwa lengo la kusitisha vurugu", ameongeza Ray.

Ufaransa kupitia wizara ya mambo ya nje imetaka kuwepo na uchaguzi " uliyo wazi na amani kwa kuheshimu Katiba", sheria muhimu kwa nchi ya Burundi.

Ubelgiji umezitaka pande zote husika katika katika uchaguzi kujizuia na kuendelea kwa vurugu, hasa kukiuka haki za binadamu, huku akionya kwa wale watakao husika na ukiukwaji wa haki za binadamu kwamba watafikishwa mbele ya mahakama za kimataifa zinazoshughulikia kesi kama hizo.

Ubelgiji umetishia kusitisha mpango wake wa ushirikiano inaofadhili kwa polisi ya Burundi kama haki za binadamu hazitaheshimishwa.

Marekani kupitia wizara yake ya mambo ya nje imesema Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu ni kinyume na Mkataba wa amani wa Arusha. 

Washington imetoa wito kwa serikali ya Burundi kuheshimu haki ya kila chama kwa kufanya maandamano, pamoja na haki ya vyombo vya habari kufanya kazi katika mchakato wa uchaguzi vikiwa huru.


Wakati huohuo raia wanaendelea kukimbilia nchi jirani ya Rwanda. Mpaka sasa wakimbizi 21,000 wa Burundi wamepewa hifadhi ya ukimbizi nchini Rwanda.

No comments:

Post a Comment