WAMILIKI wa mabasi yaendayo mikoani wameitunishia msuli Mamlaka ya
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na kusema hawatashusha nauli
kutokana na bei ya mafuta kuzidi kupanda.
Pia wamesema kama Sumatra hawatatoa majibu mapema, kuanzia Aprili 29
mwaka huu hawatokata tiketi kwa wasafiri wa mikoani badala yake
wataitisha mgomo ambao utadumu kwa siku saba.
Akizungumza katika kikao cha dharura cha Chama cha Wamiliki wa Mabasi
yaendayo mikoani (Taboa) Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho,
Enea Mrutu alisema Sumatra ilikurupuka kushusha nauli bila kufanya
mchanganuo wa kina.
Pia wamiliki hao waliafikiana kuwa yeyote atakayetoa gari lake kufanya
biashara kabla hawajapata mwafaka kutoka Sumatra watamchukulia hatua za
kisheria.
Mrutu aliitaka Serikali kurudisha viwango vya nauli za mabasi ya mikoani
kama ilivyokuwa awali kwa sababu bei ya mafuta imerudi juu baada ya
kushushwa kwa kisingizio cha bei ya mafuta kushuka.
Pia wamiliki hao walizungumzia kukithiri kwa ajali za barabarani tangu
Januari mwaka huu ambapo walijadili na kuafikiana kwamba kuanzia Mei
Mosi mwaka huu watatumia mfumo uliopendekezwa na Serikali wa kuwapo kwa
vituo maalumu vya kubadilishia madereva kwenye mabasi ya masafa marefu
kwa muda wa miezi mitatu kwa majaribio.
Vituo hivyo vitakuwa Singida kwa mabasi ya Dar es Salaam kwenda Mwanza,
Bukoba, Kahama na Kituo cha Morogoro kwa mabasi yanayokwenda mikoa ya
nyanda za juu kusini.
Uamuzi huo umechukuliwa kutokana na mapendekezo ya Jeshi la Polisi
Kikosi cha Usalama Barabarani, kuwa uchovu kwa madereva ndio chanzo
kikuu cha ajali, hivyo kuhimiza uwapo wa madereva wawili wanaopokezana
kwenye kituo kilichoteuliwa.
No comments:
Post a Comment