Sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow limemng’arisha Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila baada ya kutunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kufichua ufisadi huo uliohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika sakata hilo, mawaziri wawili walipoteza
nyadhifa zao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Ripoti ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata hilo.
Maofisa wengine kadhaa wa Serikali wamesimashwa au kufunguliwa mashtaka
kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.
Sakata hilo lililoteka kwa kiasi kikubwa mkutano
wa Bunge wa 16 na 17 kabla ya kufika bungeni, liliibuliwa na Gazeti la
The Citizen, linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd
na Kafulila kuwasilisha hoja ndani ya Bunge ili kujadiliwa.
Tuzo aliyopewa Kafulila jana na Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu unaounganisha asasi za kiraia zinazotetea
haki za binadamu (THIRD-Coalition), ni moja kati ya tuzo tatu
zilizotolewa kwa Watanzania walioonyesha ujasiri katika kutetea haki za
binadamu nchini.
Wengine ni Maanda Ngoifiko wa asasi ya kiraia,
inayotetea haki za binadamu ya PWC kutoka Loliondo wilayani
Ngorongoro, na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi, Salma Said aliyetishiwa
kuuawa baada ya kuonyesha msimamo wa kukataa shinikizo la kukubaliana
na muundo wa Muungano wa serikali mbili wakati wa Bunge Maalumu la
Katiba.
Kwa mujibu wa THIRD-Coalition, vigezo
vilivyotumika kuwapata washindi hao vilizingatia mazingira ya kazi na
hali hatarishi aliyokutana nayo mshindi wa tuzo hiyo, ikiwamo taarifa
zilizokusanywa kupitia ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za
binadamu kwa mwaka jana.
Baada ya kukabidhiwa, Kafulila alisema tuzo hiyo ni mwanzo wa hatua nyingine ya kuendelea kuibua ufisadi ndani ya Serikali.
“Nimepata ujasiri na kuamini kwamba siko peke
yangu katika vita hii, nashukuru kupata tuzo hii, lakini nashukuru zaidi
ushirikiano nilioupata kwa mhariri wa gazeti la The Citizen, ambaye
alinipatia nyaraka nne za kuanzia,” alisema Kafulila.
“Hata hivyo, ninasikitishwa kuona bado Tanesco
wakiendelea kulipia Dola 4 bilioni za capacity charge kwa kampuni hiyo
ya ITPL, wakati hukumu iliyotolewa na Mahakama ya ICSID ya Uingereza
Februari 12, mwaka jana inasema haikuwa sahihi tozo hiyo, lakini bado
kiwango hicho kinaendelea kulipiwa.”
Salma alisema pamoja na vitisho ambavyo bado
ameendelea kukutana navyo mpaka sasa kutoka kwa baadhi ya wabunge wa
lililokuwa Bunge la Katiba, bado msimamo wake utaendelea kuwa palepale.
Aidha, alisema vita iliyopo kwa sasa imehamia
kwenye harakati za Baraza la Katiba la Zanzibar ambalo linaendesha elimu
kwa Wazanzibari kuhusu Katiba Inayopendekezwa. “Mimi ni mjumbe wa
Baraza hilo na kwa sasa hawapendi kuona tukielimisha ukweli wa Katiba
hiyo na badala yake wanataka kueleza mazuri tu. Hilo tumesema
haliwezekani.”
No comments:
Post a Comment