Monday, 27 April 2015

BURUNDI KIMENUKAA ... HALI TATA MAANDAMANO ZAIDI YATAZAMIWA ...>>!!

   Askari polisi wa kutuliza ghasia wakati wa makabiliano kati ya polisi na raia Jumapili asubuhi katika mji wa Bujumbura, kufuatia kutangazwa kwa uteuzi wa Pierre Nkurunziza.

 Maandamano makubwa yanatazamiwa kufanyika leo Jumatatu nchini Burundi, hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura, baada ya watu watatu kuuawa kwa kupiga risasi na polisi katika maandamano ya jana Jumapili mjini Bujumbura.

Mashirika ya kiraia pamoja na upinzani umetolea wito raia kuingia kwa wingi mitaani Jumatatu wiki hii ili kupinga uteuzi wa rais Pierre Nkurunziza, siku mbili baada ya chama tawala cha Cndd-Fdd kumteua Nkurunziza kugombea uchaguzi wa urais kwa tiketi ya chama hicho.
Vyama vya kiraia na upinzani vinabaini kwamba uteuzi wa rais Nkurunziza wa kugombea uchaguzi wa urais ni kinyume na Katiba ya nchi ya Burundi pamoja na Mkataba wa amani na maridhiano wa Arusha, Mkaba ambao ni sheria mama ya nchi hiyo.

Vyama vya kiraia vimewataka wazazi kutoruhusu watoto zao kwenda shule, huku vikiwataka pia wafanyabiashara hususan wamiliki wa maduka kufunga maduka yao.

Vyama vya kiraia vimeinyooshea polisi kidole cha lawama kwamba imekua ikiwakamata watu usiku wa Jumapili mwishoni mwa juma hili baada ya kuwakuta nyumbani kwao.
Kwa upande wa kiongozi wa Upinzani Agathon Rwasa, amesema uamuzi huo wa rais Nkurunziza ni kinyume na katiba ya Burundi na unatishia kuiingiza Burundi katika machafuko.

Mbali na upinzani, jumuiya ya kimataifa pia haikubaliani na uwezekano wote wa rais huyo kugombea muhula wa tatu ambapo mwishoni mwa juma lililopita saa chache baada ya kuteuliwa kwake, Marekani imesikitishwa na uamuzi huo baada ya jitihada za kimataifa.

Serikali bado haijatoa tangazo lolote kuhusu maandamano hayo, lakini ilichukua uamzi tangu jana Jumapili wa kufunga mitambo ya redio tatu za kibinafsi ikiwa ni pamoja na redio Bonesha Fm, Isanganiro na RPA. Kwa sasa redio hizo hazisikiki mikoani na katika maeneo kadhaa ya nchi jirani. Serikali inazituhumu redio hizo kuwa zimekua zikirusha moja kwa moja hewani matangazo kuhusu maandamano hayo ya raia.

Hata hivyo redio zinazomilikiwa na chama tawala zimeendelea kurusha matagazo nchini nzima kuhusu maandamano hayo.

No comments:

Post a Comment