Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe, anasema; “Rais Jakaya Kikwete na CCM yake wamekwama na
atatukabidhi nchi Oktoba.”
Mbowe, ambaye yuko kwenye ziara ya kuimarisha chama katika mikoa ya
Kanda ya Ziwa, anasema kwamba kukwama kwa CCM ni kushindwa kufuata hata
ratiba ya kuteua mgombea wa chama hicho.
“Niseme jambo moja kubwa. Naomba unisikilize kwa makini. Rais Kikwete
na chama chake wamekwama. Hawawezi tena. Kwa sababu wanatafakari mgombea
atakayechuana na wa Ukawa. Hawamuoni, maana yake nini? Wanajua ni
nafasi ya Ukawa kuongoza nchi,” anasema Mbowe.
Anasema kwamba Chadema kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani
wamejipanga kushika dola, “na kwamba kama kuna watu walifikiri Ukawa ni
mchezo wa kuigiza, bali ujue wao ndiyo wanaofanya maigizo.”
Mbali ya Chadema, Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) unaundwa na
vyama vya NLD, inayoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi, CUF (Profesa
Ibrahim Lipumba) na NCCR-Mageuzi chini ya James Mbatia.
Vyama hivyo vilitiliana saini ya kushirikiana kwenye uchaguzi kwa
kuachiana maeneo ya kuwania ubunge na udiwani kulingana na nguvu ya
ushawishi.
Mbowe anasema kwamba kamwe Ukawa hawatarudi nyuma kwenye mapambano ya
kuikomboa nchi hii, iliyoshikwa na CCM na wazazi wake (TANU na ASP) kwa
zaidi ya nusu karne.
Anasema kwamba Watanzania wa sasa huwezi kuwadanganya na ndiyo maana
chama hicho kikongwe kwa sasa kinatetereka kumpata hata mgombea wakati
imebaki miezi sita kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Anasema kwamba Rais Kikwete alianza kukwama mapema kwani hata kwenye
mabadiliko ya mawaziri mwaka 2012 alilazimika kuteua makada wengine kuwa
wabunge ili awape uwaziri.
“Alimteua Profesa Sospeter Muhongo kuwa mbunge na akampa uwaziri wa
Nishati na Madini, Janet Mbene akawa Naibu Waziri wa Fedha na hata Saada
Mkuya ili naye awe Waziri wa Fedha, sasa amekwama kwenye urais,”
anasema Mbowe na kuongeza: “CCM hawana mtu wa kupambana na Ukawa.
Ikifika Oktoba ushindi ni wa Ukawa na atakabidhi nchi, na tuna matumaini
makubwa kupata ushindi.”
Anasema; “Safari hii ngoma nzito, hawa ni watani wa jadi lakini ushindi
ni wa kwetu sisi,” anasisitiza Mbowe na kwamba Watanzania wote wenye
sifa ya kupiga kura wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la
Kudumu la Wapigakura.
“Hata kama kuna wagonjwa, wabebwe kwa machela wakajiandikishe na
kuitumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kuwachagua viongozi
wawatakao,” anasema mwanasiasa huyo Mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro.
“Serikali isiruhusu wizi wa kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka
huu, ili kuiepusha nchi yetu na matatizo ya kisiasa yanayoweza
kujitokeza,” anasema Mbowe wakati anazindua kambi ya vijana katika
Kijiji cha Luhemeli, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
Hata hivyo, ameitaka Serikali kuendesha Uchaguzi Mkuu kwa uhuru na
haki na si kuendeleza vitendo vya kudhulumu haki ya wananchi, ya
kuchagua viongozi wawatakao.
Pamoja na hayo, chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi kimeieleza JAMHURI kwamba nguvu pekee iliyosalia
kwa CCM ni kutumia mabavu kuchukua madaraka — iwe ni nafasi ya urais,
ubunge au udiwani katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Kwa mujibu wa chanzo hicho ambacho kilikataa kuandikwa jina gazetini,
maofisa wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakipewa maagizo kutoka kwa viongozi
waandamizi wa CCM, kwamba wahakikishe chama hicho cha siasa kinapata
ushindi kwa njia yoyote ile hata ikiwezekana kwa nguvu ya dola.
Imeelezwa kwamba agizo hilo, ambalo limekuwa likitolewa mara kwa mara
katika vikao vya maofisa wa jeshi hilo, linaambatana na maonyo makali
ikiwa ni pamoja na kushushwa vyeo pale CCM itakapopoteza nafasi yoyote
katika uchaguzi.
“Kwa sasa hali ni ngumu mno kwa CCM kutokana na matukio mengi ya
kifisadi yanayoibuka kila kukicha na hivyo kukosa hoja yoyote inayoweza
kuwaaminisha wananchi kuwa bado inafaa kuongoza,” kimeeleza chanzo
hicho.
Imeelezwa pia anguko jingine la CCM linatokana na mnyukano mkali wa
kisiasa unaowahusu makada wake walioibuka na kujinadi mapema kuwania
nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho. Makada waliojitokeza na
kujinadi mapema kinyume na taratibu za chama hicho na kufungiwa kwa
mwaka mmoja na Kamati ya Maadili ya CCM, ni mawaziri wakuu wa zamani,
Frederick Sumaye na Edward Lowassa, ambaye amekuwa akifuatwa na makundi
mbalimbali yanayomshawishi kugombea nafasi hiyo ya urais.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira,
Naibu Waziri, Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, na
aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja.
Chadema kwa upande wao kabla ya kujiunga na Ukawa wamekuwa
wakikubalika mbele ya CCM kwa sababu ya kuingia kwenye fikra za
Watanzania na kwenye sanduku la kura.
Tangu kuanzishwa kwa Chadema miaka 23 iliyopita na kushiriki chaguzi
mbalimbali, chama hicho kimekuwa kikifanya vyema kwenye nafasi hasa za
ubunge, udiwani pamoja na viongozi wa vijiji na mitaa.
Chadema haikusimamisha mgombea wa urais mwaka 1995 hali kadhalika mwaka
2000, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni demokarsia ya kusapoti vyama
vyenye nguvu kwa nyakati hizo.
Mathalani mwaka 1995, Chadema ilimsapoti Augustino Mrema na 2000
ilimsaidia Profesa Lipumba wa CUF, lakini iliweka wagombea katika nafasi
nyingine.
Rekodi inaonesha kwamba mwaka 1995 Chadema ilipata wabunge wanne wa
majimbo na madiwani 42; wakati mwaka 2000 ilivuna wabunge watano na
madiwani 75. Katika uchaguzi huo uliofanyika kwa mara ya kwanza
uliohusisha vyama vingi baada ya miongo kadhaa, CCM ilionesha jinsi
ilivyokuwa imepoteza mvuto.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 29, 1995, mgombea wa CCM,
Benjamin Mkapa, alipata kura 4,026,422 wakati mgombea wa NCCR-Mageuzi,
Augustine Mrema, alipata kura 1,808,616. Mkapa aliyepigiwa kampeni na
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wapigakura walikuwa 6,846,681,
hivyo, Mkapa alipata asilimia 61.82 wakati Mrema akipata asilimia 27.77.
Kwa upande wa wabunge, kati ya viti 232 vilivyokuwa vinagombaniwa,
CCM ilipata 186 sawa na asilimia 80.17 huku NCCR-Mageuzi ikipata 16 sawa
na asilimia 6.9 ya viti vilivyogombaniwa. Mwaka 2000 katika uchaguzi wa
pili na wa kwanza bila ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kuwapo, CCM
ilifanya vizuri zaidi kuliko miaka mitano nyuma.
Rais Mkapa akiingia ngwe ya pili alipata asilimia 71.74 ya kura zote
za urais (5,863,201), wakati Prof. Lipumba wa CUF akipata asilimia 16.26
ya kura za urais (1,329,077) na Mrema akigombea kwa mara ya pili
akipata kura 637,077.
Wapigakura waliojiandikisha walikuwa 10,088,484 na waliopiga kura
wakiwa 8,517,598 sawa na asilimia 84.4. Kwa upande wa Bunge, kwenye
uchaguzi huo CCM ilipata viti 202 kati ya viti 231 vilivyogombaniwa
wakati CUF ikipata viti 16.
CCM iliongeza asilimia yake kutoka asilimia 80.17 na kufikia asilimia
87.45. Idadi ya kura za wabunge iliongezeka kutoka asilimia 59.22 miaka
mitano iliyopita kufika asilimia 65.19 wakati kwa CUF walipunguza
kutoka asilimia 21.83 hadi asilimia 12.54.
Mwaka 2005, katika uchaguzi ambao CCM ilimteua Jakaya Kikwete kama
mgombea wake, alionekana kuwa mshindi mapema kwa sababu alionekana
kubeba matumaini makubwa. Wapigakura waliojiandikisha walikuwa
16,401,694 na waliojitokeza kupiga kura walikuwa 11,875,927 sawa na
asilimia 72.4. Kikwete alipata kura 9,123,952 sawa na asilimia 80.28.
Prof. Lipumba wa CUF aliyejaribu bahati hiyo kwa mara ya tatu
mfululizo, alipata kura 1,327,125 wakati Freeman Mbowe wa Chadema
akipata kura 668,756 sawa na asilimia 5.88.
Kwa upande wa wabunge CCM iliendelea kufanya vizuri zaidi. Kati ya viti
232 vilivyokuwa vinagombaniwa CCM ilipata viti 206 wakati CUF ikipata
viti 19 na Chadema vitano. CCM ilipata asilimia 69 ya kura za wabunge
wakati CUF ikipata asilimia 14 na Chadema ikipata asilimia 8.20.
Mwaka 2010 Chadema ilichukua nafasi ya NCCR-Mageuzi na CUF ambavyo
vilikuwa ndivyo vikibeba kombe la wapinzani. Ulipofika Uchaguzi Mkuu wa
2010, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 20,137,303. Hii ilikuwa ni
mara 2.3 ya waliojiandikisha kupiga kura mwaka 1995.
Hata hivyo, idadi ya waliojitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi ule
ilikuwa ni 8,626,283 sawa na asilimia 42.8 wakati mwaka 2005
waliojitokeza kupiga kura wakiwa asilimia 72.4 mwaka 2010 ilipungua
asilimia 29.6.
Rais Kikwete alipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 62.83 wakati Dk.
Willibrod Slaa, mgombea wa Chadema akipata kura 2,271,941 sawa na
asilimia 27.05 ya kura za urais huku Prof. Lipumba (akijaribu kwa mara
ya 4) akipata asilimia 8.28 ya kura za urais.
Kutoka kura 9,123,952 alizopata mwaka 2005 hadi kura 5,276,827 ni
anguko kubwa kwani alipoteza angalau kura 3,847,125. Hata hivyo, Dk.
Slaa, ambaye hakuwahi kugombea urais kabla, alipata kura hizo hapo juu
akiinyanyua Chadema kuliko ilivyokuwa kwa Mbowe mwaka 2005.
Kwa upande wa wabunge kati ya viti 239 vilivyokuwa vinagombewa, CCM
ilipata viti 186, CDM ilipata viti 23 wakati CUF ikipata viti 24.
Matokeo ya 2010 yanaakisi kwa namna ya ajabu matokeo ya 1995 wakati
mwamko wa upinzani wa vyama vingi uliporudishwa na kushirikishwa kwenye
uchaguzi.
Hali kadhalika, wakati Rais Kikwete akitetea nafasi yake mwaka 2010,
Chadema ilivuna jumla ya wabunge 49 wakiwamo 23 wa majimbo na madiwani
467; na katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki ikaongeza
kiti kimoja cha Joshua Nassari.
Mwaka 1995, Mkapa alishinda kwa asilimia 61.82, mwaka 2010 Kikwete
alishinda kwa asilimia 62.83 wakati huohuo mwaka 1995 Mrema (Upinzani)
alipata asilimia 27.77 mwaka 2010 Dk. Slaa alipata asilimia 27.05.
Mwaka 1995, mshindi wa tatu, Profesa Lipumba, alipata asilimia 6.43,
wakati 2010 mshindi wa tatu (Lipumba) alipata asilimia 8.28 wakati mwaka
1995 kati ya viti 232 vilivyogombewa CCM ilipata 186 mwaka 2010 kati ya
viti 239 vilivyogombewa, CCM ilipata viti 186.
Mwaka huo wa 1995, chama kikuu cha upinzani nchini CUF kilipata viti
24, mwaka 2010 chama kikuu cha Upinzani nchini Chadema kilipata viti 23.
Kadhalika, Mbunge wa zamani wa Musoma, Paul Ndobho, amezungumzia hali
ya sasa ya CCM na kusema; “Ni hatari kubwa kwa CCM kwani inazidi
kukataliwa ndani ya fikra za Watanzania na zaidi sana imezidi kukataliwa
kwenye sanduku la kura.”
Ndobho anasema kwamba matokeo hayo hususani yale ya uchaguzi wa
marudio yanaonesha, licha ya CCM kushinda, bado inazidi kukataliwa na
maelfu ya Watanzania, na kwamba kuanzia uchaguzi wa 2010 na chaguzi
ndogo zilizofuatia, zinaonesha hadi hivi sasa CCM bado inazidi
kukataliwa na hilo ni jambo la hatari.
“Hata pale ambako inashinda, bado inashinda kwa tofauti ya kura
chache ikilinganishwa na huko nyuma. Tatizo ni ufisadi, lakini CCM bado
haijapata majibu ya kuzuia kukataliwa kwake,” anasema Ndobho.
Matokeo ya uchaguzi katika maeneo ya vijiji na vitongoji, CCM ilipata
ushindi wa asilimia 79.81 (vijiji) na 79.83 katika vitongoji, wakati
kwenye mitaa ambayo ipo sehemu za mijini ilishuka zaidi na kupata
asilimia 66.66, ikilinganishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1999,
ambako ilipata asilimia 89.2 katika mitaa, asilimia 91 katika vitongoji
na asilimia 91.6 katika vijiji.
Katika uchaguzi wa mwaka jana, CCM ilipata vijiji 7,290 ikifuatiwa na
Chadema yenye vijiji 1,248. CUF ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na
vijiji 946 ikifuatiwa na UDP yenye vinne na TLP na NLD vyenye viwili
kila kimoja.
Katika nafasi za wenyeviti wa mtaa, CCM imechukua jumla ya mitaa
2,116. Vyama vingine na nafasi zao kwenye mabano ni Chadema (753), CUF
(235), ACT (9), NCCR-Mageuzi (8) wakati vyama vya TLP, UMD, UDP na NRA
vimepata mtaa mmoja kila kimoja.
No comments:
Post a Comment