Tuesday, 28 April 2015
KAULI HII NI YA NAPE NA RAFIKI ZAKE AU CHAMA CHA MAPINDUZI CCM?? PANGA LIPO PALE PALE ...
Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, anasema kwamba kada yeyote atakayepatikana na hatia ya kukiuka maagizo au taratibu za Chama Cha Mapinduzi (CCM), atachujwa tu.
Kadhalika, amesema kwamba kwa watakaokatwa majina, wakatathmini na kuona kuwa hawakutendewa haki, wanaruhusiwa kuondoka kuhamia vyama vingine au kuacha siasa.
“Siku zote nimekuwa nikisema na ninasema CCM ni chama kikubwa ambacho kinaendeshwa kwa misingi, si chama kinachoweza kuyumbishwa na mtu mmoja,” anasema Nape.
Nape anasema kuwa CCM imekuwa na utaratibu wa kufanya mchujo katika chaguzi zake zote zilizotangulia, hivyo utaratibu huo utaendelea kutumika bila kuhofia kupoteza baadhi ya wanachama wake.
Anabainisha; “Tumewahi kuchuja watu tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, suala la kuhofia mtu mmoja kuwa akiondolewa atapasua chama ni upuuzi unaokuzwa na vyombo vya habari na watu wachache wasioijua CCM.”
Katika mahojiano maalum na JAMHURI, Nape amesisitiza kwamba utaratibu wa kuchuja majina ya makada wenye dosari uko palepale.
Kadhalika Nape anaeleza kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kutoka CCM ikapasuka, kwani chama hicho ni mali ya Watanzania si mtu mmoja anayejidanganya kuwa ana nguvu.
Msemaji huyo wa chama anasema kuwa siyo kwamba vyama vya upinzani vimeanza kuwinda wagombea kutoka CCM mwaka huu, bali ni kawaida kuwa baadhi ya vyama vya upinzani vimekuwa vikiwawinda baadhi ya makada wa CCM hata baada ya mchujo lakini wamekuwa hawajiungi na vyama hivyo.
“Hao tuliowahi kuwachuja miaka ya nyuma mpaka sasa mbona hawajaondoka? Na si kwamba walikuwa hawawindwi, wanawindwa nasi tunafahamu lakini ni uamuzi wao wenyewe. Ila CCM ipo imara na haiyumbishwi na vitu vidogo vidogo,” anasema.
Anasema CCM inatarajia kumtangaza rasmi mgombea wake siku ya kumtangaza ikifika, na hadi sasa hawajaamua utaratibu wa utakaotumika.
Kauli ya Nape inakuja siku chache kabla ya chama hicho kuwa na vikao vyake vya ndani kupanga ratiba ya Kamati Kuu (CC) itakayopanga ajenda za Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu chama hicho (NEC).
Taarifa kutoka ndani ya CCM zinasema kwamba chama hicho kimelazimika kuwa na vikao hivyo muhimu vya ndani, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha tarehe rasmi ya kupigia kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa.
Kwa mujibu wa sheria na taratibu na matangazo ya Ikulu, kura ya maoni kwa Katiba hiyo ilikuwa ifanyike Alhamisi ijayo ambayo ingekuwa Aprili 30, mwaka huu.
Lakini Tume ya Uchaguzi imekwama kukamilisha kazi ya kusajili wapigakura kwa wakati, hivyo kulazimisha CCM nayo kupangua ratiba yake ya vikao vya ndani kuwapata wagombea wake.
Wiki iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kifungo cha vigogo sita wanaowania urais ndani ya chama hicho kutokana na kuanza kampeni kabla ya muda kufika, kuwa kanuni za uchaguzi za chama hicho zitawameza makada wake wanaotumia fedha kuwanunua wapigakura kama maandazi.
Mangula anasema kuwa kanuni za chama hicho zinaruhusu mwanachama kutangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, lakini haziruhusu kuanza kampeni kabla ya muda.
Anasema kuwa wanatambua ya kuwa wapo wanachama wanaotoa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha, ila anawaonya kuacha mambo hayo maana chama kina macho, kinawaona na kitachukua hatua muda utakapofika.
Anaeleza kuwa kamati ya maadili ya chama hicho iliwabana kwa maswali magumu makada walioanza kampeni kabla ya muda, hivyo kujikuta wakishindwa kujitetea kutokana na kile ambacho wameanza kukifanya na wao kubaki midomo wazi.
Anabainisha kuwa walibaki midomo wazi kutokana na mahojiano hayo kuambatanishwa na ushahidi wa makosa waliyoyafanya ikiwa ni pamoja na shughuli walizozifanya.
Mangula anasema kuwa Kamati ya Maadili ilipowaita katika mahojiano walioneshwa siku, tarehe na saa ikiwa ni pamoja na fedha walizotoa wakati wakifanya kampeni kabla ya muda.
Februari mwaka jana, Kamati Kuu ya CCM iliwafungia kwa miezi 12 vigogo wa chama hicho kwa kuanza kampeni kabla ya wakati na kukiuka maadili ya chama.
Waliopata adhabu hiyo ni mawaziri wakuu wastaafu Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Kilimo, Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment