Tanzania jana iliadhimisha miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar huku viongozi wa upinzani wakisusia sherehe hizo za mwisho katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete ambazo, makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walitia fora.
Rais Kikwete alikagua gwaride hilo katika sherehe zilizofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na
viongozi mbalimbali pamoja na maelfu ya wananchi
ambao baadhi walilazimika kutumia Uwanja Mkuu wa Taifa kufuatilia
shughuli hizo.
Baadhi ya viongozi hao ni pamoja na, Makamu wa
Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein,
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim
Seif Sharrif Hamad. Wengine ni Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Rais
mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Waziri Mkuu
Mstaafu, Frederick Sumaye.
Wapinzani wasusia
Viongozi wakuu wa vyama vya upinzani hawakushiriki
maadhimisho hayo baadhi wakiwa mikoani katika shughuli za kuimarisha
vyama vyao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe yuko mkoani Kagera na Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye yuko mkoani Mtwara.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia, Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe hawakuhudhuria na
sababu za kutokuwapo kwao hazikuelezwa.
Wakuu waliokosekana
Pia, baadhi ya viongozi wa kitaifa hawakuonekana
katika sherehe hizo akiwamo Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan
Mwinyi, Mawaziri wakuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba, John
Malecela, Salim Ahmed Salim, Cleopa Msuya Edward Lowassa.
Kikwete uwanjani
Kama ilivyo kawaida, msafara wa Rais Kikwete
aliyekuwa na Mkuu wa Majeshi, Davis Mwamunyange katika gari maalumu la
jeshi lililozungukwa na magari mengine saba na pikipiki 15, ulizunguka
uwanja huku kiongozi huyo akipunga mkono na kushangiliwa kwa nguvu.
No comments:
Post a Comment