Thursday, 23 April 2015
VILABU NA TIKETI ...
*West Ham wapunguza bei ya zile za msimu
*Baadhi wakataa kushusha, wengine ‘bubu’
Ligi Kuu ya England (EPL) kwa misimu ijayo inatarajiwa kupigwa jeki na kiasi kikubwa cha fedha kutokana na dili za matangazo ya televisheni.
Hali hiyo imezua taharuki miongoni mwa washabiki, maana ilielezwa kwamba fedha hizo zitarudi kwa njia mbalimbali, mojawapo ikiwa ni nyongeza ya bei ya tiketi, bidhaa na huduma zinazohusiana na ligi na televisheni.
Wakati West Ham wametangaza kwamba watapunguza bei ya tiketi kutokana na dili hizo nzuri klabu inazopata pamoja na Bodi ya Ligi, klabu nyingine zimeonekana kutia pamba masikioni.
West Ham, maarufu kama ‘The Hammers’ watatoa tiketi ya bei rahisi zaidi kwa msimu mzima – £289 watakapohamia Uwanja wa Olimpiki unaobeba watazamani 54,000 kutoka waliko Upton Park unaochukua watu 35,000.
Hiyo itakuwa ni msimu wa 2016-17 hata hivyo, si msimu ujao. Kwa sasa, tiketi rahisi zaidi katika Ligi Kuu kwa msimu ni £299 – kutoka kwa mabingwa watetezi, Manchester City.
West Ham wanasema kwamba punguzo la bei hizo limesababishwa na mkataba wa miaka mitatu wa pauni bilioni 5.13 unaovunja rekodi ya historia ya EPL, ambapo kutoka kwenye fungu hilo, klabu zitafaidi kimapato.
Makamu Mwenyekiti wa West Ham, Karren Brady ameiambia BBC Radio 5 kwamba anapokaa kwenye mikutano ya Bodi ya EPL mjadala mkubwa ni juu ya kufanya watu wamudu kuingia kwenye soka.
“Mie huingia mle kwenye mikutano … lakini siwezi kuzisemea klabu nyingine. Tunahisi kwamba tunao wajibu wa kusaidia hili,” anasema.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo bei hizo zimeshushwa ili waweze kujaza uwanja mpya na mkubwa zaidi watakaokuwa wakitumia, alikana, akisema hawauzi bidhaa ya kiwango cha chini kwa bei pungufu bali bidhaa bora zaidi kwa bei nafuu.
Hata hivyo, viongozi wa klabu nyingi miongoni mwa 19 zilizobaki walipoulizwa juu ya suala la kupunguza tiketi, ama walisema hazijafanya uamuzi huku baadhi wakidai walishashusha siku zilizopita.
Arsenal, kwa mfano, walisema walikuwa wameshafanya uamuzi juu ya suala hilo kwa msimu ujao na wanaendelea na jitihada kutoa makumi ya maelfu ya tiketi hizo.
Wanaongeza kwamba tiketi yao ya msimu ni kwa mechi 26.
Burnley wanasema hawana mpango wa kupunguza bei na kwamba lazima kuwe na uwiano baina ya mapato kwa timu na uwezo wa kupunguza bei.
Chelsea wanasema wao hupitia upya bei za tiketi kila msimu, lakini hawakusema iwapo watashusha bei msimu ujao au 2016/17.
Hull, kinyume na matarajio, wanasema kwamba bei za tiketi kwa wakubwa na wazee zimeongezeka kwa 6% kwa msimu ujao na kwamba bado hawajaweka mipango kwa msimu unaoufuata.
Newcastle wanasema dili za sasa zinatoa nafasi kwa washabiki kusaini dili za muda mrefu ambapo wanapata unafuu wa bei.
Tottenham Hotspur wanasema hawana mipango ya kupunguza bei kabla ya kuhamia kwenye uwanja mpya wanaotarajia kuanza kujenga karibuni.
Southampton kadhalika wanasema hakuna kitu kama hicho kwa sasa kuhusiana na msimu wa 2016/17 na Stoke pia hawana nia hiyo.
Sunderland wanadai kwamba tiketi zao ni kati ya zilizo rahisi zaidi kwenye ligi za juu na kwamba msimu uliopita walipunguza bei.
Vipi kwa Swansea? Wanasema wao ndio walikuwa wa kwanza kutangaza kupunguza bei ya tiketi za msimu tangu Desemba hivyo wanashangaa kusikia West Ham ndio wamefungua pazia.
“Tulipunguza kwa £10 kwenye tiketi zote za msimu licha ya kwamba tiketi zetu ni bei rahisi sana kwa ujumla na hakuna inayozidi £489.
West Bromwich Albion hawana mpango kama huo, wakisema itategemea na hadhi ya ligi yenyewe.
Manchester City wanasema tayari wana tiketi ya bei ya chini zaidi – £299 kwa msimu kwa hiyo hakuna nia ya kupunguza zaidi kwa msimu wa 2016-17.
Manchester United nao wanasema hawatarajii uamuzi wowote kabla ya kuanza kwa mwaka ujao wa fedha, yaani Juni 30.
Kuna timu ambazo hazikutoa majibu; nazo ni Aston Villa, Crystal Palace, Everton na Liverpool.
Leicester walichosema ni kwamba huwa hawashiriki katika utafiti wa aina hii wakati Queen Park Rangers (QPR) walikataa kutoa maoni yoyote, wakisema; “no comment.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment