RAIS Jakaya Kikwete jana aliongoza maelfu ya Watanzania kuadhimisha sherehe za miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, huku vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama vikiwa kivutio kikubwa.
Tofauti na ilivyozoelekea miaka yote ambako vikosi vya ulinzi na usalama huwa vinakuwa kundi moja tu vikiwa vimevalia sare maalumu za sherehe, jana kulikuwa na makundi mawili tofauti yakiwa na zana nyingi na za kisasa zinazotumika katika utendaji wa kila siku wa shughuli za jeshi.
Kundi la kwanza lilikuwa na gadi saba ambalo lilikuwa limevalia sare za sherehe na muda wote lilikuwa katikati ya Uwanja wa Uhuru.
Kundi la pili lilikuwa nje ya Uwanja wa Uhuru likiwa na gadi 13 na kati ya hizo, moja ilikuwa na kikundi maalumu cha askari wa wanamaji na makomandoo ambao muda wote walikuwa wakionyesha zana wanazotumia katika shughuli za vita.
Kikosi cha askari wa anga walipita mbele ya Amirijeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete wakiwa na vifaa maalumu vya mawasiliano, kitu ambacho hakijawahi kuonekana katika sherehe zilizopita katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa mara ya kwanza katika sherehe hizo, kulionekana kikundi cha Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) wanawake, ambao walionekana kuwa kivutio kwa maelfu ya wananchi.
Kila gadi iliyokuwapo uwanjani hapo, ilikuwa na askari 50, wanawake wakiwa 25 na wanaume 25.
VIONGOZI WANENA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya viongozi wastaafu wa Serikali, walisema Muungano unapaswa kuigwa na mataifa mengine.
Walisema vijana wana nafasi kubwa ya kuuenzi na kuendeleza Muungano ili udumu miaka 50 ijayo.
“Sisi tumestaafu, tunawaachia vijana waweze kuuendeleza, hivyo basi wanapaswa kuunga mkono na kuudumisha ili udumu miaka 100,”alisema Spika mstaafu, Pius Msekwa.
Alisema licha ya Muungano huo kupitia kwenye mawimbi yaliyoibua kero, mpaka sasa yameweza kushughulikiwa na kubakishwa mambo machache ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi.
Msekwa alisema ili kuonyesha Muungano ni jambo la muhimu, ametunga kitabu maalumu ambacho kimeelezea mambo mbalimbali yanayohusu muungano na misingi imara ya kuuenzi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema Muungano umeleta mafaniko makubwa katika nyanja mbalimbali zikiwamo za uchumi na jamii.
Alisema Watanzania wanapaswa kuuenzi na kuudumisha.
Alisema kipindi hiki cha kuelekea kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu, vijana wengi wanapaswa kujitokeza wajiandikishe na kupiga kura.
“Ushiriki wa vijana kwenye kupiga kura kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa ni muhimu kwa sababu inaweza kusaidia katika uchaguzi mkuu,”alisema Butiku.
HALAIKI
Katika maadhimisho hayo pia vilikuwapo vikundi maalumu vya wanafunzi(halaiki) ambao walioonyesha maumbo mbalimbali ya zana za kivita na wengine wakiwa wameshika bunduki.
Maumbo hayo yalikuwa na ujumbe mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi kudumisha amani na utulivu na kuendeleza shughuli mbalimbali za maendeleo. Pia yalikuwapo maonyeshao ya ndege vita ambazo zilipita kwa mwendo wa pole na wa kasi.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omary Makungu, Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha na Spika mstaafu, Pius Msekwa.
Wengine ni Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Taifa Zanzibar, Seif Sharif Hamad , Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
AKAMATWA
Wakati huohuo, mtu mmoja ambaye jina lake halikufahamiska mara moja, alikamatwa na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kujifanya Ofisa wa Usalama wa Taifa.
Kijana huyo alisimama kwenye lango kuu huku akionekana kuongoza wananchi waliokuwa wanaingia uwanjani hapo.
Kutokana na hali hiyo, mmoja wa askari waliokuwa karibu walimshtukia na kuwaita maofisa usalama ambao walimkamata na kumhoji ndipo ilipobainika ni ‘ofisa feki’.
Taarifa zinasema kijana huyo aliwahi kuajiriwa na JWTZ kabla ya kufukuzwa kwa utovu wa nidhamu.
No comments:
Post a Comment