Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuandikisha wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM na kwamba ile yenye upinzani itaandikishwa kwa kulipua ili watu wengi wenye sifa ya kupiga kura wasiandikishwe.
NEC ilianza kuboresha Daftari la Wapigakura kwa
kuandikisha wananchi wa Mkoa wa Njombe, ambako watu 300,080
waliandikishwa kati ya 392,634 waliotarajiwa na sasa inaelekea mikoa ya
Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa baada ya kupokea mashine nyingine 1,600.
Kazi hiyo itaendelea kwenye mikoa ya Katavi, Mbeya na Dodoma wakati
mashine 1,600 zaidi zitakapowasili.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva
amesema hilo ni jambo jipya kwake kwa kuwa hawakuangalia suala hilo
wakati wa kupanga mikoa hiyo.
Akizungumza jana kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kuwasili nchini akitokea
Marekani, Dk Slaa alisema wamegundua kwamba mwishoni mwa kazi ya
uandikishaji kwenye mikoa ambayo ni ngome ya vyama vya upinzani, watu
wengi hawataandikishwa.
“Tumegundua hujuma zao, NEC wameanza kuandikisha
wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM. Huko wanajitahidi
kuandikisha wapigakura wote na wanachukua muda mrefu,” alisema Dk Slaa
akionekana kurejea Mkoa wa Njombe ambako NEC imetumia takriban miezi
miwili kuandikisha wapigakura.
“Mikoa yenye ngome ya Chadema na vyama vingine vya
upinzani itakuwa ya mwisho kuandikisha wapigakura na uandikishaji huo
utakuwa wa harakaharaka ambao utawaacha mamia ya watu bila kuandikishwa
kwa sababu muda utakuwa hautoshi,” alisema Dk Slaa.
Alisema suala hilo linaweza kuvuruga uchaguzi, hasa ikizingatiwa kwamba mchakato wa uandikishaji umekuwa na sintofahamu nyingi.
Kwa mujibu wa matokeo ya urais katika Uchaguzi
Mkuu wa 2010, CCM ilivuna kura 128,809 katika majimbo matatu ya mkoani
Njombe (Njombe, Ludewa na Makete) wakati huo ukiwa ndani ya Mkoa wa
Iringa. Chadema ilifuatia kwa kupata kura 36,928 na CUF/NCCR zilipata
kura 1,670
Kwa kujumuisha kura hizo na majimbo mengine ya Iringa CCM ilipata jumla ya kura 299,799 ikifuatiwa na Chadema iliyopata kura 76,010. CUF na NCCR-Mageuzi zilipata jumla ya kura 3,137. Hadi sasa upinzani una mbunge mmoja tu kwenye mikoa hiyo miwili, Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini.
Kwenye uchaguzi wa Rais mwaka 2010 mkoani Lindi,
mgombea wa CCM alipata kura 150,118 akiwa mbele ya mgombea wa CUF
aliyepata kura 64,875 wakati wagombea wa Chadema na NCCR walipata jumla
ya kura 12,880. Wapinzani wana wabunge wawili mkoani Lindi ambao ni
Selemani Bungera wa Kilwa Kusini na Salum Barwany wa Lindi Mjini, wote
kutoka CUF.
Mkoani Mtwara, mgombea urais wa CCM alipata kura
213,844 akimuacha mbali mgombea wa CUF aliyepata kura 81,953, huku
wagombea wa Chadema na NCCR wakipata jumla ya kura 82,233. Hakuna mbunge
kutoka upinzani mkoani Mtwara.
Takwimu za 2010 pia zinaonyesha kuwa mkoani
Ruvuma, mgombea urais wa CCM alipata kura 198,090, akimuacha kwa mbali
mgombea wa Chadema aliyepata kura 36,044, CUF (28,873) na NCCR kura 397.
No comments:
Post a Comment