Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amesema kanuni za uchaguzi za chama hicho zitawameza makada wake wanaotumia fedha kuwanunua wapigakura kama maandazi.
Mangula alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na
wanaCCM wa Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam katika ziara yake katika
majimbo mawili ya Ukonga na Segerea.
Mangula alisema wapo wagombea wanaodhani kuwa wao
ni maarufu na wanasahau kuwa fedha walizotanguliza mbele ndiyo maarufu
na siyo wao wenyewe, hivyo wanajidanganya.
“Unatawanya fedha kila kona, kwa kila kundi,
halafu unajiita maarufu badala ya kuona fedha zako ndiyo maarufu...
unajidanganya ukijua kuwa unajidanganya,” alisema.
Aliwataka wanachama hao kuwa makini na watu wenye
tamaa ya kwenda Ikulu, huku akinukuu alichowahi kukisema Baba wa Taifa,
Mwalimu Nyerere kuwa; “mtu yeyote anayetafuta kwenda Ikulu kwa fedha
muogopeni kama ukoma.”
Akifafanua maadili na kanuni za wagombea wa CCM,
Mangula anayeongoza pia Kamati Ndogo ya maadili, alisema, “Yeyote
anayekukuruka kuutafuta uongozi kwa kutumia fedha, kununua wanachama ili
apigiwe kura au apitishwe, akiona jina lake halikutoka ajue limemezwa
na kanuni na sheria za uchaguzi.”
Kauli hiyo ya Mangula imekuja wakati kamati ya
maadili anayoiongoza ikiendelea kuwachunguza makada sita wa chama hicho
kwa madai ya kuanza kampeni mapema na kufanya vitendo vinavyokiuka
maadili.
Alisema CCM ni umoja, hivyo wanaoleta migogoro ni
watu waliopotoka ambao wanashindwa kutekeleza sheria walizojiwekea na
wenye tamaa ya madaraka.
Mangula alisisitiza kuwa anayowaeleza makada hao
si hadithi, bali ni ya kweli na yaliwahi kufanyika huko nyuma akitolea
mfano mwaka 2000 akiwa Katibu Mkuu wa CCM walipowasimamisha wagombea wa
majimbo ya Morogoro ambao wagombea sita walihonga, uchunguzi ukafanyika
ilipobainika walisimamishwa wote na wahusika wakapigwa marufuku
kugombea.
Alisema hata mkoani Singida makada waliobainika kusambaza fedha ili wachaguliwe walitimuliwa na nafasi ikatangazwa upya.
“Wakalalamika demokrasia ipo wapi, tukawajibu hakuna cha demokrasia, unalazimisha vipi demokrasia kwa kutumia fedha?” alisema.
Alisema kutumia fedha kwenye uchaguzi ni tatizo
sugu, hadi watendaji wanakula rushwa kwa wagombea mpaka wanafikia
kupanga hadi bei ya hongo.
No comments:
Post a Comment