\
Kundi hatari la vijana limeibuka wilayani mwanga mkoani Kilimanjaro na
kuzua hofu. Kundi hilo la vijana wapatao 40, wanadaiwa kupewa mafunzo ya
kijeshi na watu wasiofamika wilayani humo.
Vijana hao kwa muda wa miezi kadhaa inadaiwa wamekuwa wakipewa mafunzo
ya kijeshi katika vijiji vya Lang’ata na Kirya kwa lengo la kuandaliwa
kufanya matukio ya kihalifu nchini.
Habari za uhakika kutoka wilayani Mwanga zinasema hali hiyo imezua
wasiwasi mkubwa kwa wananchi ambao walipiga simu polisi kuomba msaada.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga, alikiri kuwapo taarifa hizo.
“Taarifa hizi nimezisikia tangu juzi, tunazifanyia kazi, sina uhakika,
sina cha kusema kwa sasa. “Tumesambaza askari karibu maeneo yote hadi
muda huu tunaongea wapo doria wanaendelea na msako mkali,” alisema
Ndemanga.
Alisema polisi na vyombo vingine vya dola wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wanakuwa salama.
“Nakuhakikishia ndugu yetu, askari wetu wanafanya kazi usiku na mchana,
tunataka kuona wananchi wanabaki salama na wanaendelea na kazi zao kama
kawaida,” alisema.
Alisema hadi jana wakazi wa eneo la Lang’ata na Kirya wamekuwa wakipiga
simu polisi kuomba msaada kutokana na uwepo wa kundi hilo la vijana
wanaopewa mafunzo yanayodaiwa kuwa huenda yanaweza kuwa chanzo cha
kuibuka kwa matukio ya kigaidi nchini.
“Wananchi wanapiga simu na kutwambia kuna watu, lakini mwenyewe
nimekwenda hadi huko sikufanikiwa… naomba uwe na subira nitawajulisha
maendeleo ya msako huu,” alisema Ndemanga.
Habari zinasema eneo la Lang’ata ambalo liko karibu na Bwawa la Nyumba
ya Mungu, limezungukwa na pori ambalo linaweza kutumiwa na wahalifu.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Godfrey Kamwela, alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, alisema hana taarifa lakini akaomba apewe muda wa
kulifuatilia.
“Ndiyo nimesikia kwako, naomba unipe muda kidogo nilifuatilie, maana
hatuwezi kupuuza taarifa zinazotufikia,” alisema Kamanda Kamwela.
Matukio ya vijana kupewa mafunzo ya kijeshi na hata kudaiwa kuandaliwa
kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, yamekuwa yakijitokeza kila
wakati nchini.
Oktoba 7, mwaka 2013, Jeshi la Polisi mkoani Mtwara liliwashikilia watu
11 kwa tuhuma za kupata mafunzo ya kijeshi msituni kwa kutumia CDs za
al-Shabaab.
Tukio hilo la aina yake lilitokea katika Mlima Makolionga, Wilaya ya
Nanyumbu mkoani humo ambapo pia CDs zenye mafunzo v 8mbalimbali ya
kijeshi 25 zilikamatwa.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen, alisema watuhumiwa hao
walikamatwa baada ya jeshi lake kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.
“CD hizo zilikuwa zinatoa mafunzo ya Al-Shabaab ya kuchinja watu, mauaji
ya Osama bin Laden, Zindukeni Zanzibar, Kuandaa Majeshi, Mauaji ya Idd
Amin na Mogadishu Sniper,” alisema Zolothe.
Alisema watuhumiwa wote ni wakazi wa Wilaya ya Nanyumbu na kwamba
walikuwa wakiongozwa na Mohamed Makande, 39, mkazi wa Kijiji cha
Sengenya ambaye pia alikamatwa.
Vitu walivyokamatwa navyo watuhumiwa hao ni mapanga mawili, deki ya DVD,
solar, visu, tochi, betri, simu za kiganjani 5, vyombo mbalimbali vya
kulia chakula, baiskeli tatu, vitabu mbalimbali vya dini ya Kiislamu,
unga wa mahindi kilo 50, mahindi kilo 150 na virago vya kulalia.
Vingine ni mfuko wa kijani unaosadikiwa ni wa kijeshi wenye nembo ya
nanga ya meli yenye mistari kulia na kushoto na nyoka katikati.
No comments:
Post a Comment