Wednesday, 1 April 2015

UCHAGUZI WA NIGERIA FUNZO KWA TANZANIA ..>>

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wananchi wa Nigeria walipiga kura kumchagua Rais katika uchaguzi wenye ushindani mkali kati ya Rais wa sasa, Goodluck Jonathan na mpinzani wake Jenerali Muhamadu Buhari.

Katika makala haya, mtangazaji na mwandaaji wa vipindi katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Salimu Kikeke anazungumzia uzoefu alioupata katika mchakato wa uchaguzi huo, kama alivyohojiwa na mwandishi wetu.

Swali: Tueleze uzoefu wako kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa kuandikisha wapigakura na pengine changamoto zake ulizozibaini nchini Nigeria?

Jibu: Nadhani dunia inaelekea katika mfumo wa kidijitali na itafika wakati pengine kila nchi duniani itakuwa ikitumia mfumo wa kielektroniki, katika uchaguzi, lakini pia katika mambo mengine mbalimbali.

Kwa kuwa bado ni mfumo mpya, watu wengi hawajaweza kuelewa hasa unafanyaje kazi. Nadhani uzuri wa mfumo huu, ni kwamba una uwazi zaidi na matokeo yake yanaweza kuaminiwa na wapiga kura kwa kuwa ni mashine ambazo hufanya kazi na hilo pia hupunguza uwezekano wa makosa ambayo huweza kufanywa na binadamu.

Vifaa vya kusomea kadi (card readers) vina betri yenye uwezo wa kufanya kazi kwa saa 14, na husoma kadi moja kwa chini ya sekunde 60 na ni vigumu ‘kuchakachua’ labda mtu aghushi ‘VIN,’ yaani namba maalumu ya mpigakura.

Kwa hiyo mfumo huu una ufanisi mkubwa, lakini kama teknolojia nyingine zozote mpya, zina changamoto zake siku za mwanzo, na zinapozoeleka hali inakuwa tofauti.

Swali: Kipi kimekukosha na kukusononesha kuhusu mchakato mzima wa uandikishaji na uendeshwaji wa kampeni nchini Nigeria?

Jibu: Hii ni moja ya nchi zinazoelezwa kuwa na demokrasia kubwa barani Afrika. Pia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mingi, uchaguzi huu una ushindani mkali kati ya wagombea urais ambao ni Goodluck Jonathan wa chama tawala PDP na Jenerali Muhhamadu Buhari wa chama cha upinzani APC, wanavutana vikali kabisa.

Kitu ambacho kimenivutia hasa ninapozungumza na wananchi wa hapa, ni kutaja suala la amani. Licha ya vuta nikuvute iliyopo, wengi wanasema cha msingi ni kufanya uchaguzi huu kwa amani. Kumekuwa na vijembe vya hapa na pale, na wakati mwingine ghadhabu ambazo unaweza kudhani zitavuka mipaka na kuleta tafrani, lakini hilo halijajitokeza kwa kiwango kikubwa cha kutisha- ukiacha matukio ya Desemba mwaka jana, ambapo kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya haki za Binadamu watu takriban 58 waliuawa katika ghasia zinazihusiana na uchaguzi katika sehemu mbalimbali.

Pamoja na kuwa masuala makuu kama usalama, ufisadi na uchumi ni mambo yanayozungumzwa zaidi kwenye vyombo vya habari, wananchi wengi wa kawaida wanataka mambo ya kila siku maishani kama vile umeme na maji, lakini kubwa kuliko yote wanataka amani.

Kampeni kwa jumla zimekuwa salama na kwa kuwa kuna ushindani mkali katika urais, wagombea wamekuwa wakijinadi kwa kusema kinagaubaga jinsi watakavyokabiliana na changamoto za taifa hili. Jambo zuri pengine ni kuwa wote wamewahi kuongoza taifa hili.

No comments:

Post a Comment