Wednesday, 22 April 2015

UCHUMI WA KATI HAUJENGWI KWA ''POROJO'' ... >>

Kuna dhana potofu hapa nchini kuhusu nishati ya gesi ambayo imegunduliwa kwa wingi katika maeneo mbalimbali nchini. Dhana hiyo ni kuwa, kugunduliwa kwa nishati hiyo ni neema kwa nchi yetu, kwani sasa kila mwananchi anapaswa kukaa ‘mkao wa kula’. Wananchi wameaswa kujiweka sawa tayari kwa kusema ‘kwa heri’ kwa umaskini. Wengine wamehamasishwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hivi karibuni akiwa katika ziara yake nje ya nchi kwamba atakuwa rais wa mwisho kuongoza nchi maskini, kutokana na kupatikana kwa rasilimali kubwa ya gesi na uwezekano wa kuwapo hazina kubwa ya mafuta.
Hivyo, fikra za wananchi wengi zimeelekezwa katika kuaga umaskini na ‘kula kuku kwa mrija’. 

Wameaminishwa kwamba kutokana na kupatikana kwa gesi, nchi yetu itaupiga teke uchumi duni hivi punde na kujenga uchumi wa kati kama zilivyofanya baadhi ya nchi kama Malaysia, Singapore, Indonesia na Korea Kusini, ambazo zilikuwa maskini kama sisi wakati tunapata uhuru mwaka 1961.
Wapi tulikosea kiasi cha kuendelea kuogelea katika umaskini uliopitiliza ni swali gumu kulitolea maelezo katika safu hii kutokana na ufinyu wa nafasi. Itoshe tu kusema kuwa, pamoja na nchi hizo kutokuwa na rasilimali nyingi kama ilivyo Tanzania, zimefanikiwa kujenga uchumi wa kati kwa kufanya mapinduzi ya viwanda wakizingatia teknolojia ya kisasa.
Tunapozungumzia kugunduliwa kwa gesi na mafuta nchini hatuna maana kwamba siyo jambo jema kwa nchi yetu na wananchi wake. Tunachojaribu kusema ni kwamba kupatikana kwa gesi au mafuta hakuna maana au manufaa yoyote iwapo Serikali na wananchi hawatajitayarisha kwa kila namna kupokea ujio wa rasilimali hizo muhimu katika ujenzi wa uchumi. Zipo nchi barani Afrika na kwingineko ambazo zimejaaliwa hazina kubwa ya rasilimali ya gesi na mafuta, lakini si tu zimebakia katika umaskini wa kupindukia, bali pia nishati hiyo imegeuka kuwa balaa, imeleta vita, vurugu na umwagaji damu.
Ni jambo la kawaida sasa kuona baadhi ya nchi hizo zikiwa katika migogoro isiyokwisha, ikiwa ni pamoja na vita ya wenyewe kwa wenyewe, kwani mgawanyo wa mapato ya rasilimali hizo unawanufaisha wachache. Sera na mikataba mibovu ya gesi na mafuta na ukosefu wa uwazi katika kutekeleza sera hizo vimesababisha vitendo vya ufisadi na rushwa. Nchi hizo hazitawaliki. 

Ndio maana tunasema kupatikana kwa gesi na mafuta katika nchi yetu hakuwahakikishii wananchi moja kwa moja kwamba watapata neema kama Serikali haitaweka mazingira mazuri, uwazi, sera na mipango endelevu itakayosimamia rasilimali hiyo.
Hivyo, uchumi wa kati unajengeka katika jamii inayojitambua na yenye mwelekeo. Jamii iliyotayarishwa kisaikolojia na yenye uzalendo, yenye kuona uchungu na rasilimali za nchi, yenye kulinda miundombinu. Vinginevyo, hata ikiletwa treni ya Delux au mradi wa mabasi yaendayo kasi vitakongolewa. Ni kweli gesi na mafuta ni vichocheo vya maendeleo, lakini lazima iwepo rasilimali watu iliyoelimika, iliyostaarabika, yenye nidhamu, maadili na inayofanya kazi kwa bidii.
Hivyo ndivyo Malaysia na wenzake walivyojenga uchumi wa kati. Katika kuitayarisha jamii kwa ujio wa gesi na mafuta, Serikali sasa lazima ijipange kuwekeza katika elimu, ijenge viwanda na kutengeneza ajira. Uchumi wa kati unajengwa kwa vitendo kwa jamii kufanya kazi kwa bidii, si kwa dhana ya ‘kula kuku kwa mrija’.

No comments:

Post a Comment