Wednesday, 1 April 2015

VURUGU ZA ZANZIBAR CCM WATAKA TUME HURU KUUNDWA ..>>

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimeitaka Serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya wafuasi 25 wa Chama cha Wananchi (CUF), waliokuwa wanatoka katika mkutano Makunduchi hivi karibuni.
Kauli hiyo ya CCM imekuja siku chache baada ya CUF, kuishutumu kuhusika na tukio la kupigwa na kujeruhiwa kwa wafuasi wake.


 Akizungumza na MTANZANIA jana mjini Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai, alikana chama chao kuhusika na kutukio la kupigwa kwa wafuasi hao wa CUF.

 Vuai alisema ili kuondoa mkanganyiko huo uliojitokeza, ni vema Serikali ikaunda tume huru ambayo itafanya uchunguzi wa kina wa suala hilo kuliko ilivyo sasa ambapo kila chama kinavutia upande wake.
“Hivi sasa kila mmoja anasema lake, kwa hali hii ni vema Serikali ikaunda tume huru ambayo itafanya uchunguzi ili ukweli ujulikane nani aliyeusika na tukio hili ambapo itasaidia kumaliza chuki na visasi vinavyopandikizwa na viongozi wa CUF kwa wananchi kuwa CCM ndiyo iliyohusika na suala hili.
“Kwa sasa Zanzibar inapita katika wakati ambao tuliusahau, matukio na vitendo vya uvamizi na kuwajeruhi watu hadi kupoteza maisha sasa vinaonekana kushamiri kwa kasi, hili si sawa hata kidogo, nasi CCM tunalani kitendo hiki,” alisema Vuai.

 Alisema tabia iliyoanza kuota mizizi visiwani humo kwa vyama vya siasa kuanza kutuhumiana kwa kuhusishana katika matukio ya kihalifu si jambo jema kwa mustakabali wa siasa za Zanzibar na watu wake.
“Kutokana na udhaifu uliopo miongoni mwetu kama wanasiasa, inawezekana wakatokea watu wana visasi binafsi vyao mtaani wakasubiri mazingira fulani ili wafanye uhalifu wao wa kisasi na kisha lawama zikaja CCM.
“CCM inajua wajibu wake wa kulinda amani na utulivu na hili tuliahidi mbele ya wananchi kuwa tutalinda amani na si vinginevyo, ila kwa kuwa CCM ndiyo inatawala, si vema kila jambo ikatupiwa lawama za kila aina zikiwamo za matukio ya kihalifu,” alisema.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria wa CUF, Pavu Abdallah, alisema kwa sasa hali ya majeruhi waliolazwa hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu inaendelea kuimarika.
“Juzi tulitaka kuwasafirisha majeruhi wanne ambao hali zao hazikuwa nzuri, lakini madaktari wa Hospitali ya Mnazi Mmoja walisema wana uwezo wa kuwatibu, kwa hali hiyo tunaheshimu uamuzi wao.
“Kutokana na majeraha waliyopata, tulihitaji wakapatiwe matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako kuna vifaa na madaktari wa kila aina, licha ya madaktari kudai kuwa majeruhi hao watatibiwa Zanzibar lakini wengine wamepewa huduma ya kwanza pekee badala ya matibabu na hali zao haziridhishi,” alisema Pavu.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Khamis Juma Khamis, Abdillah Abas Khamis, Shamis Ali Khamis na Juma Kassim Masoud ambao kutokana na hali zao walitakiwa kusafirishwa kupelekwa katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

No comments:

Post a Comment