KUDHOOFU kwa afya ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima ambaye wiki moja iliyopita alizimia wakati akihojiwa na Polisi,
kumezua utata.
Wakati baadhi wakijenga hisia kwamba hatua hiyo huenda ikawa ina mkono
wa Mungu, au imetokana na kuvurugika kwa mfumo wa kawaida wa ufahamu,
hata hivyo maofisa wa Jeshi la Polisi wa Kituo Kikuu Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam waliofika kumuhoji Gwajima ambaye aliwasili kituoni hapo
akiwa mzima wa afya, wamenyooshewa kidole.
Daktari anayemtibu Askofu Gwajima, Photunatus Mazigo, akizungumza na
MTANZANIA Jumamosi licha ya kusema maadili hayamruhusu kutaja ugonjwa
wake, hata hivyo alieleza kuwa askofu huyo ana maumivu makali katika
mguu na mkono wa upande wa kushoto.
“Askofu Gwajima ana maumivu makali katika mguu na mkono wake wa kushoto
pamoja na mgongoni, sisemi kuwa huo ndio ugonjwa wake ila inawezekana
ikawa hivyo.
“Maumivu hayo huenda ndiyo yalisababisha kushindwa kupanda ngazi
aliporudi Polisi kuhojiwa na tulivyomruhusu sio kwamba alikuwa amepona
kwa asilimia mia moja, ndio maana tulimpatia kiti (wheel chair) kwa
ajili ya kumsaidia,” alisema Dk. Mazigo.
Ingawa Daktari wake huyo hasemi maumivu hayo yametokana na nini, kauli
yake hiyo imejenga hisia kwa baadhi kwamba kile kilichotendeka polisi
ndio msingi wa maumivu yake hayo.
Kwa mujibu wa Daktari wa Gwajima, pamoja na kwamba walimruhusu Askofu
huyo, lakini walimshauri kupumzika wiki moja kutokana na kwamba alikuwa
hajapona kikamilifu bali alikuwa ana nafuu tu.
“Tulipomruhusu kurudi nyumbani tulimwambia baada ya wiki moja arudi
kuripoti hospitali kwa ajili ya kuchunguza afya yake,” alisema Dk.
Mazigo.
Alisema ugonjwa wake sio kwamba ni siri au haujulikani, lakini matatizo
aliyoyapata yalimwathiri na kusababisha kukosa nguvu katika mguu na
mkono wake wa kushoto.
“Siwezi kusema kuwa ugonjwa wake ni nini kwa sababu maadili hayaruhusu,
lakini siku akiniruhusu nieleze nitasema, hata yeye mwenyewe anajua
ugonjwa wake mnaweza kumuuliza.
Zaidi, Dk. Mazigo alisema, Gwajima alipofika katika Hospitali ya TMJ
alikuwa katika hali mbaya, hivyo kulazimika kumpeleka katika chumba cha
uangalizi maalumu (ICU).
Katika chumba hicho alikaa kwa muda wa siku tatu na baada ya kuona kuwa
hali yake imebadilika walimhamishia katika wodi ya kawaida.
“Tulimhamisha kutokana na kwamba tuliona hali yake inaendelea kuimarika
na baada ya kumfanyia mazoezi tuliona kuwa akipata msaada anaweza
kusimama mwenyewe ndio maana tukampatia kiti hicho,” alisema.
Daktari mwingine aliyezungumza na gazeti hili ambaye hakutaka kutajwa
jina lake gazetini, alisema hawezi kusema moja kwa moja kama maumivu
hayo ni dalili za ugonjwa fulani na kwamba jambo hilo linaweza kupatiwa
ufumbuzi na uchunguzi wa kitaalamu.
“Wengi wamekuwa wakihusisha dalili hizo na ugonjwa wa kiharusi, lakini
siwezi kusema moja kwa moja mpaka kuwe na majibu ya uchunguzi wa
kitaalamu,” alisema daktari huyo.
Hata hivyo, alisema watu wenye historia nzuri kwa maana wasio na
magonjwa kama shinikizo la damu huwa si rahisi kupata ugonjwa wa
kiharusi.
“Kwa hiyo siwezi kusema moja kwa moja, hapa cha muhimu Gwajima mwenyewe
awe wazi, lakini pia uzoefu unaonyesha wazi kwamba intelijensia ya
polisi mara nyingi kama si wakati wote huwa inakuwa ni ya kutumia
nguvu,” alisema Daktari huyo.
Wakati Daktari huyo akisema hayo, Msemaji wa Dk. Gwajima, Mchungaji
Yekonia Behanaze, alikaririwa na MTANZANIA Jumapili wiki iliyopita
akisema kuwa, askofu huyo hajawahi kuwa na shinikizo la damu.
Awali, mwanasheria wa Gwajima, John Mallya, alisema hali ya mteja wake
ilikuwa nzuri lakini hawezi kuzungumzia ugonjwa unaomsumbua.
“Mimi nimezungumza naye asubuhi alikuwa akiendelea vizuri lakini siwezi
kuzungumzia ugonjwa wake ni vyema mkamtafuta daktari wake,”alisema
Mallya.
Mtaalamu wa magonjwa ya binadamu kutoka Hospitali Teule wilayani Muheza
Mkoa wa Tanga, Aubrey Maonga, alisema hali iliyomkuta Gwajima inaweza
kusababishwa na mshtuko wa neva za fahamu au moyo kushindwa kupokea damu
inayorudi kutoka mwilini.
“Inategemea alikuwa katika mazingira ya aina gani, lakini hali ile
inaweza kusababishwa na mshtuko wa neva za fahamu (neurogenic shock)
kama alisikia jambo ambalo hakulitegemea. Hatujui walikuwa wakizungumza
nini hadi ashtuke vile.
“Inawezekana pia ni tatizo la damu kutoka sehemu ya chini ya mwili
inayotakiwa kurudi kwenye moyo kushindwa kurudi, kwa hali hiyo mtu
anaweza kuzimia. Hali hiyo huwakuta watu wanaosimama kwa muda mrefu hasa
wanajeshi. Lakini kwa kuwa alikuwa anahojiwa, inawezekana ni mshtuko wa
neva za fahamu,” alisema Dk. Aubrey.
Askofu Gwajima aliitwa kwa mara ya kwanza na jeshi hilo Machi 27, baada
ya kutoa kauli ya kumkashifu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar
es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo, kuhusu waraka wa Jukwaa la
Wakristo.
Hata hivyo, wakati akihojiwa katika mahojiano hayo yaliyodumu kwa
takribani saa saba, alizimia na hivyo kupelekwa katika Hospitali ya
Polisi Kurasini na baadaye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kabla ya
kuhamishiwa Hospitali wa TMJ ambako alitibiwa na kuruhusiwa baada ya
siku tatu.
Jeshi la Polisi lilimwita tena kwenye mahojiano Aprili 2 na alipofika
Kituo Kikuu cha Polisi Kanda ya Dar es Salaam, hali yake iliendelea kuwa
mbaya kiasi cha kushindwa kupanda ngazi za kuingia kituoni hapo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani
Kova, juzi alisema hawakuweza kumhoji Askofu Gwajima ili kumpa fursa
afya yake iimarike zaidi.
Kova alisema, Askofu Gwajima alifika Kituo Kikuu cha Polisi
akisindikizwa na wasaidizi wake ikiwa ni pamoja na wakili wake saa mbili
asubuhi.
“Alifika kituoni akiwa bado anatumia kiti cha magurudumu matatu (wheel
chair) na alikubaliana na wapelelezi kwamba akaendelee na matibabu.
“Gwajima anatakiwa kurudi kuripoti Aprili 9 mwaka huu ili aweze
kuendelea na mahojiano kuhusu tuhuma za kumkashifu na kumtukana Askofu
wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo,” alisema Kova.
Gwajima atoa madai mazito...
Akizungumza na waumini wake siku moja kabla ya kurudi Polisi, Gwajima
ambaye kwa maelezo yake mwenyewe aliwahi kuugua kiasi cha kushindwa
kutembea kwa miaka sita kabla ya kuokoka, alidai kuna mtu anayemhujumu
na kwamba hatafanikiwa.
Alisema, Mungu aliyemwezesha kutembea ndiye atakayemponya tena.
“Najua kinachoendelea. Namwombea mtu mmoja ambaye yuko hapa, nasema
nakufahamu vizuri, nakujua vizuri na ninasema hutafanikiwa kwa jina la
Yesu,” alisema huku waumini wakijibu ‘ameeen’.
“Nakwambia hutafanikiwa. Usifurahi leo kuniona nimekaa kwenye kiti hiki,
bado nina maumivu, bado sina nguvu lakini nimesema lazima leo niende
nyumbani mwa Bwana. Wewe ni mtoto mdogo, hujatoka mbali,” aliongeza
Gwajima.
“Huyo aliyenifanya nitembee, hawezi kuniacha nikae kwenye kiti hiki
tena. Unatakiwa ujue unashindana na mtu aliyewahi kuwa hatembei, lakini
Mungu akamtoa kwenye kiti kama hiki. Ole wako wewe unayelazimisha
kumrudisha mtu wangu pale, nakwambia sitakaa pale unapofikiri nikae,”
alisema.
Aliwataka waumini wake kumsindikiza kituo cha polisi siku aliyohitajiwa kuripoti.
“Kwa hiyo nawaomba watu wote bila kuacha hata mmoja kwa wingi wenu,
twende kwa pamoja kule polisi makao makuu, ili muweze kuona kwa ukaribu
sana. Lipo jambo nililoliona na nimelisikia linaendelea lakini
hawatashinda, asema Bwana wa majeshi, amen,” alisisitiza Gwajima huku
akishangiliwa na waumini wake.
Hata hivyo, alipotafutwa kwa njia ya simu ili kufafanua kuhusu kauli
yake hiyo, simu yake iliita bila kupokelewa kwa muda mrefu. Juhudi za
gazeti hili kumtafuta Gwajima bado zinaendelea.
No comments:
Post a Comment