Saturday, 4 April 2015
MALI ZA ZITTO KABWE UBAONI ...
UKWASI wa Kiongozi Mkuu wa Chama Cha Alliance for Change and Transparency(ACT Wazalendo), Zitto Kabwe umeongezeka kutoka umiliki wa shamba moja na Sh milioni 30 alizokuwa amezihifadhi katika akaunti za benki mbili tofauti hapa nchini, na sasa anamiliki mali na fedha zinazofikia Sh milioni 690, MTANZANIA Jumamosi linaripoti.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mpya alizoziweka hadharani wiki hii katika fomu maalum ya kuonyesha mali zinazomilikiwa na viongozi wa chama hicho, Zitto ametanabaisha kuwa kwa sasa anamiliki nyumba mbili.
Nyumba hizo, moja ina thamani ya Sh milioni 180 na nyingine Sh milioni 43, Pia anamiliki kitalu cha ekari 12 ambacho kinathamani ya Sh milioni 25, vyote vikiwa Mwandiga mkoani Kigoma.
Zitto pia ameweka hadharani kumiliki mashamba matatu katika mikoa ya Kigoma, Mtwara na Dar es Salaam.
Katika ufafanuzi wake kuhusu mashamba hayo, Zitto ameeleza kuwa anamiliki shamba la ekari sita katika manispaa ya mji wa Mtwara likiwa na thamani ya Sh milioni 60.
Hali kadhalika shamba lingine la ekari tatu lenye thamani ya Sh milioni 20 huko Matyazo Kigoma, lingine la ekari 3 lenye thamani ya shilingi milioni 90 ambalo liko Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Katika fomu hiyo, Zitto alijaza kuwa anamiliki pia gari moja aina ya Land Lover, Free Lander ambalo alinunua kwa dola za Kimarekani 40,000 sawa na Sh. milioni 72.
Kwa upande wa fedha alizokuwa nazo wakati anajaza fomu hiyo ni Sh. milioni 18, pia alitanabaisha kuwa amehifadhi fedha katika Benki ya CRDB, NMB na STANBIC zenye jumla ya Sh milioni 9.8.
Zitto pia aliweka wazi kumilika shirika lisilo la kibiashara la Kigoma Development Initiatives ambalo linaumiliki wa vitalu vya maili 25 huko Ilogelo wilaya ya Uvinza.
Pamoja na hilo pia anamiliki Kampuni ya Gombe Advisors ambayo inahisa asilimia 25 katika Kampuni ya Leka Dutigite.
Zaidi ameeleza kuwa ameanza kuchangia mfuko wa Hifadhi za Jamii(NSSF), tangu mwaka 2004.
Mbali na hilo la ukwasi, Zitto alieleza bayana juu ya madeni aliyoyakopa kwa nyakati tofauti wakati akiwa mbunge, ambayo yana jumla ya Sh. milioni 174.6.
Kwa nyakati tofauti, Zitto amekuwa akihusishwa na kuwa na ukwasi wa hali ya juu yakiwamo magari ya kifahari jambo ambalo amekuwa akilikanusha.
Mwaka 2012 alikaririwa na vyombo vya habari pasipo kutaja thamani, alisema kuwa anamiliki nyumba yenye vyumba viwili huko Kigoma.
“Sijawahi kuwa na nyumba wala kiwanja hapa Dar wala Dodoma isipokuwa nyumbani Kigoma, huko nina nyumba ya vyumba viwili tu ambayo niliijenga wakati wa uchaguzi baada ya wazee kunishauri kuwa siyo vizuri kuendelea kutumia nyumba ya baba yangu…Nina akaunti mbili tu moja benki ya NMB na nyingine benki ya CRDB na zote hazina fedha zaidi ya shs Mil. 15 kila moja.” Alikaririwa wakati huo.
Pia alitoa utetezi wake wa umiliki wa magari, ambapo alisema kuwa anamiliki gari aina aina ya Land Lover, Free Lander pamoja na gari dogo aina ya Toyota Vista.
“Baada ya kuwa mbunge , nakumbuka April 2007 niliingiza nchini gari aina ya Hammer na nadhani nilikuwa mtu wa pili kuingiza gari hilo hapa nchini, Kaka yangu Salum anayefanya biashara ya magari ndiye aliyeniletea na hili sikuliendesha zaidi ya wiki mbili, likanishinda. Lilikuwa la kifahari mno, nikamwambia alichukue aliuze na hela yangu anirudishie,” alikaririwa Zitto.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment