Sunday, 5 April 2015

KENYA YAAPA KULIPIZA KISASI BAADA YA SHAMBULIO LA AL SHABAAB ..

Wakati Wakiristo duniani, wakiadhimisha siku ya Pasaka hivi leo nchini Kenya maombolezo ya kitaifa ya siku tatu yameanza baada ya kuawa kwa wanafunzi 147 waliovamiwa na kundi la kigaidi la Al Shabab kutoka nchini Somalia wakiwa katika Chuo Kikuu cha Garissa Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Bendera zinapepea nusu mlingoti na leo siku ya Pasaka inatumiwa nchini humo kuomboleza na kuwakumbuka wale wote waliofariki katika shambulizi hilo.

Rais Uhuru Kenyatta amesema, serikali yake italipiza kisasi dhidi ya kundi hilo la Al Shabab nchini Somali kwa mauaji iliyotekeleza.

Kenyatta ameongeza kuwa wale wote wanaosaidia kupanga mashambulizi nchini humo na kuwafadhili magaidi hao pia watakiona cha mtema kuni.

                                  Jamaa ndugu na marafiki wakiomboleza
Magaidi wanne waliokivamia chuo hicho siku ya Alhamisi asubuhi waliuliwa na miili yao iliwekwa hadharani hapo jana ili wananchi wajionee huku polisi wakiwakamata washukiwa watano wanaohusishwa na shambulizi hilo.

Chuo Kikuu cha Garissa kimefungwa na serikali imetoa mabasi kuwasafirsiha wanafunzi zaidi ya mia sita makwao baada ya kutokea kwa shambulizi hilo.

 
Maafisa wa Idara za huduma za Dharura wakimuokoa mwanafunzi aliyejeruhiwa katika shambulio dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa, shambulio ambalo limedaiwa kutekelezwa na kundi la Al Shebab kutoka Somalia.
 
Mashambulizi ya Garissa yamelaaniwa na viongozi wa dunia, akiwemo kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis.

Rais wa Marekani Barrack Obama amesema kuwa, nchi yake itaendelea kuisaidia Kenya kupambana na ugaidi.

Mauaji ya Garrisa ndio mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini Kenya tangu shambulizi la kigaidi dhidi ya Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi mwaka 1998.

                    Wanajeshi wakilinda usalama nje ya Chuo Kikuu cha Garrisa

No comments:

Post a Comment