Wednesday, 8 April 2015

UCHUNGUZI WA BAINI SABABU ZA KUTOKWISHA AJALI ZA BARABARANI ...>>

Ajali za vyombo vya usafiri wa majini na barabarani huenda zikaendelea kutokea nchini na kuchukua uhai wa watu wengi zaidi kila kukicha kutokana Serikali kuwaadhibu madereva tu na kuwaacha maofisa waliohusika na miundombinu mibovu na wanaoshindwa kukagua ipasavyo vyombo hivyo.

Kila zikitokea ajali za barabarani, Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani hukimbilia kuwakamata madereva na kuwafungulia mashtaka na wakati mwingine wamiliki wa vyombo hivyo, lakini siyo maofisa waliosababisha barabara kujengwa chini ya kiwango, nyembamba au kuacha mashimo bila kuyafukia wala maofisa wanaoacha kukagua magari.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, kwa muda mrefu sasa, unaonyesha kwamba, Serikali imekuwa ikishituka tu wakati wa vifo na viongozi wakihudhuria mazishi ambako hutoa makaripio na ahadi ya kuwachukulia hatua madereva wanaodaiwa kuwa wazembe na kuwawajibisha watendaji wote ambao hawafanyi lolote kuzuia majanga ya ajali. Lakini huwa hakuna ufuatiliaji, hata kesi zikitupwa, Serikali huishia kuahidi kukata rufaa bila utekelezaji.

Kwa ajali za barabarani, Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama Barabarani hukimbilia kuwakamata madereva na kuwafungulia mashtaka, lakini wanaosababisha vifo katika matukio kama ya milipuko ya mabomu au kuacha nyaya za umeme zikiwa zimelala barabarani hadi kusababisha ajali hawachukuliwi hatua ambayo ni sawa na waliosimamia ujenzi wa barabara nyembamba.

Takwimu za vifo

Wakati dawa ya kudhibiti ajali haijapatikana, takwimu za Usalama Barabarani zinaonyesha kuwa mwaka 2012 kulikuwa na ajali 11,438 zilizosababisha vifo vya watu 4,919; mwaka 2013 idadi ajali ilikuwa 11,311 zilizosababisha vifo vya abiria 1,739 na mwaka jana ajali zilikuwa 8,405 na vifo vilikuwa 1,743.

Kila vinapotokea vifo vya watu kutokana na ama kulipuliwa na mabomu, ajali ya vyombo vya usafiri wa majini, barabarani au kukanyaga umeme, Serikali hutoa kauli nzito na kuahidi kumchukulia hatua kali mtu yeyote atakayebainika kuhusika kuonyesha kuwa haitavumilia uzembe wa aina yoyote lakini baada ya muda, hali hubaki ileile bila ufuatiliaji.

Nani alaumiwe?
Mkurugenzi mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), Ahmed Kilima anasema ajali za barabarani zinasababishwa na mazingira makubwa matatu ambayo ni makosa ya kibinadamu, ubovu wa miundombinu na ubovu wa magari.
Kilima anataja makosa ya kibinadamu kuwa ni mazingira ya uzembe wa dereva, ulevi, utoaji wa leseni kwa madereva wasiokuwa na ujuzi wa kutosha, ukaguzi mdogo wa mabasi na malori yanayosafiri mikoani, abiria kushabikia mwendo kasi na udhaifu wa wamiliki wa mabasi na malori kuajiri madereva wasio na uwezo.
“Kwa hiyo, siwezi kusema nani alaumiwe lakini mazingira yanaonyesha madereva na wamiliki wanahusika zaidi kwa upande wao kabla ya kuangalia makosa mengine yanayotokana na mamlaka husika,” alisema Kilima.
Katibu Mkuu wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), Godwin Ntongeji anasema ili kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la ajali nchini, ni lazima ukaguzi wa mabasi na madereva ufanyike mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment