Wednesday, 8 April 2015
VIBALI VYA WAGANGA WA KIENYEJI KUSITISHWA SAME ..> by MTANZANIA
SERIKALI wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro, imesema itafanya tathmini ya vibali vyote vya waganga wa jadi vilivyokwisha muda wake.
Pamoja na tathmini hiyo, pia uongozi utasimamisha kwa muda utoaji wa vibali vipya vya waganga wa jadi.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Katibu Tawala Wilaya ya Same, Mashauri Msangi alipozungumza kwenye maadhimisho ya siku ya ulemavu wa ubongo duniani.
“Tutafanya tathmini ya vibali na tutasimamisha vibali vipya bila hofu ya kurogwa kwa vile tutafanya hivyo kupambana na mauaji ya albino.
“Kazi hiyo itasimamiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kwa kufuatilia vibali vyote vya waganga na tutaanza kuwa makini na waganga wageni wanaoingia katika wilaya yetu.
“Tunaamini hatua hii itasaidia kujua waganga wasiotambuliwa kisheria kwa sababu hao ndiyo
wanaotuchafulia jina la nchi yetu katika sura ya kimataifa,” alisema Msangi na kuongeza:
“Wilaya ya Same kijiografia ni tofauti na wilaya nyingine za Mkoa wa Kilimanjaro ikizingatiwa imezungukwa na milima mirefu na wananchi wake wanategemea kilimo, ufugaji na biashara mbalimbali kujipatia kipato.
“Kwa hiyo tunaomba wananchi watupe ushirikiano katika vita hii kwa vile wanawafahamu waganga wanaochochea kwa namna fulani mauaji ya albino,” alisema.
Naye Ofisa Elimu wa Elimu Maalumu, Wilaya ya Same Marietha Shayo, aliwataka wazazi na walezi wasiwafiche majumbani watoto wenye matatizo ya ubongo kwani nao ni binadamu kama binadamu wengine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment