Wednesday, 8 April 2015
MARAFIKI WA LOWASSA WATEMBELEA YATIMA ..>
ZAIDI ya vijana 200 wa 4 U Movement Friends of Lowassa wametembelea watoto yatima katika kituo cha kulelea watoto cha Save Africa kilichoko Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha na kutoa zawadi ya Pasaka kwa watoto hao.
Kabla vijana hao hawajatembelea kituo hicho na kula chakula na watoto hao, walitembea kwa maandamano kutoka eneo la Usa River hadi kituoni hapo.
Wakati wa matembezi hayo, walikuwa wakiimba nyimbo za kumsifu Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuonyesha nia yao ya kumtaka agombee urais mwaka huu.
Pia, mara kadhaa walikuwa wakiimba nyimbo za wasanii mbalimbali huku wakisema kaulimbiu yao ni safari ya matumaini, simama uhesabiwe.
Akizungumzia uamuzi wao huo, Mratibu kundi hilo, Aziz Mfundo, alisema lengo la kutoa msaada kwa watoto hao na maandamano waliyoyafanya ni kuhamasisha na kumuomba Lowassa agombee urais mwaka huu kwa kuwa wanaamini ana uwezo wa kuiongoza Tanzania.
Pia, alisema wanatarajia kutembelea makundi maalum mbalimbali na kutoa misaada kwa makundi hayo ili wahusika wasijione wametengwa na jamii.
“Tutaendelea kutoa misaada na kama Lowassa atachaguliwa kuwa rais tutakuwa tumempata mtu wa kuwawezesha vijana kupata ajira kupitia sekta ya viwanda,” alisema Mfundo.
Naye Rehema Mroso kutoka kundi hilo la 4 U Movement, alisema wamelazimika kutoa msaada huo kama sehemu ya kutambua mchango wa Lowassa katika taifa hili.
“Lowassa ni mpenda watu na sisi ni wapenda watu ndiyo maana tumeamua kuwatembelea watoto hawa na kuwapa zawadi. Kwa hiyo, tunawaomba Watanzania wamuunge mkono Lowassa atakapotangaza nia kwa sababu tunaamini ndiye jembe pekee lenye uwezo wa kuiongoza nchi hii,” alisema Mroso.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment