Saturday, 21 February 2015
CLOUDS HAIUZWI .. ASEMA KUSAGA ..!!
MKURUGENZI Mtendaji wa Clouds Media Group, ambayo inamiliki Kituo cha Redio cha Clouds, Joseph Kusaga, amesema taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinazoeleza kuwa redio hiyo imeuzwa kwa mfanyabiashara mwenye ukwasi mkubwa hapa nchini, Rostam Aziz, siyo za kweli.
Kusaga aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kuhusu kusambaa kwa taarifa hizo na kueleza kuwa habari hizo ni uzushi unaopaswa kupuuzwa. Kusaga alisema taarifa za kuuzwa kwa Redio Clouds zimetengenezwa na watu walioamua kupoteza muda wao katika mitandao ya kijamii huku wenzao wakivuna fedha nyingi kupitia njia hiyo ya mawasiliano (social media). “Clouds Media Group ni kampuni iliyoanzishwa nchini kwa ushirikiano wa watu wengi, hivyo kuamua kuiuza kiholela ni jambo la kushangaza, ingawa pia si dhambi kufanya hivyo kwa mtu yeyote kwa sababu ni biashara kama zilivyokuwa biashara nyingine. “Naomba Watanzania wote wapuuze habari hizo na wenzetu walioamua kuitumia mitandao ya kijamii vibaya waache, kwa sababu kumhusisha Rostam na uongo huu ni jambo la kushangaza,” alisema Kusaga.
Alisema Redio Clouds ni chombo huru kisichofungamana na chama chochote cha siasa na kitatoa haki kwa vyama vyote na wanasiasa wakati wa kampeni zinazotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu. “Huu ni mwaka mgumu, hivyo naomba niseme ikitokea suala la kuhoji au kuunga mkono siasa basi haki itatolewa kwa wanasiasa wote, ukizingatia kwamba chombo chetu hakina chama cha siasa inachokiunga mkono kwa sababu zozote zile,” alisema Kusaga.
Clouds Media Group inamiliki kituo cha Radio cha Clouds FM, Clouds Tv na Choice FM.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment