Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema Serikali imepanga kuajiri walimu zaidi ya 35,000 kwa ajili ya shule za sekondari ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu nchini.
Pinda alisema hayo juzi mjini Iringa alipokuwa
akihutubia mamia ya wakazi wa Kata ya Kiwere, Tarafa ya Kalenga, baada
ya kukagua ujenzi wa maabara na kuzindua nyumba nne za walimu wa shule
hiyo.
Alisema walimu hao watagawanywa kwenye shule
kulingana na mahitaji yaliyowasilishwa kuwataka wahusika kuzipa
kipaumbele shule ambazo miundombinu yake imekamilika, ikiwamo vyumba vya
maabara.
Akifafanua kuhusu kasi ya ujenzi wa maabara,
Waziri Mkuu alisema: “Mkoa mzima wa Iringa unahitaji kuwa na maabara 318
na zilizo tayari ni 108. Lakini kuna nyingine 141 ambazo zimekwishaanza
kujengwa na zimefikia hatua nzuri. Nimeambiwa katika muda mfupi ujao
kutakuwa na maabara 249 zilizokamilika.
“Mkuu wa mkoa inabidi uwasukume watu wako ili hizi
69 ambazo bado hazijaanza kujengwa zikamilike kabla ya Juni, mwaka huu,
kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Alisema hataongeza
tena muda wa ujenzi,” alisema Pinda.
Alisema elimu ni sekta ya msingi ambayo Serikali
imeamua kuipa umuhimu wa kipekee na kuiweka katika moja ya maeneo sita
muhimu ya kipaumbele chini ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Aliwataka wanafunzi wa shule hiyo wasome kwa bidii na wawe wasikivu ili waweze kufanya vizuri zaidi kwenye masomo yao.
Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Ofisa
Elimu wa Wilaya ya Iringa, Leonard Msigwa alisema ujenzi wa nyumba nne
za walimu zitakazokaliwa na familia nne kila moja, umegharimu Sh323.2
milioni.
Alisema nyumba hizo zenye vyumba vitatu vya kulala, sebule na jiko,
Msigwa alisema nyumba hizo zimejengwa na Shirika
la DESWOS la Ujerumani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya
Iringa na wananchi.
Akifafanua kuhusu hali ya ujenzi wa maabara, Ofisa
Elimu huyo alisema hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya
masomo ua kemia na baiolojia na tayari mfumo wa gesi na maji
umekwishafungwa ndani ya vyumba hivyo.
No comments:
Post a Comment