Kamati Kuu ya CCM (CC) inakutana Jumamosi wiki hii huku mambo muhimu sita yakitarajiwa kujadiliwa, likiwamo suala la makada wa chama hicho waliopewa adhabu ya onyo kali kwa kuanza kampeni za urais mapema na ukiukaji wa maadili.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, licha ya kutoeleza
ajenda za kikao hicho, ilisema kitafanyika jijini Dar es Salaam na
kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kuanzia saa 4 asubuhi.
Kikao hicho kinafanyika wakati upepo wa kisiasa
ndani ya chama hicho ukiwa haujatulia huku kukiwapo masuala mazito ya
kitaifa yanayotikisa medani za kisiasa, likiwamo suala la uandikishaji
wapiga kura, maandalizi ya kura ya maoni za kupitisha Katiba
Inayopendekezwa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambayo
yameelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa hayawezi kukwepeka katika kikao
hicho.
Adhabu kwa wagombea
Itakumbukwa kuwa kikao hicho kitafanyika ikiwa ni
siku 10 baada ya kukamilika tarehe ya mwisho ya adhabu kwa makada sita
wa CCM, waliokuwa wakitumikia adhabu ya miezi 12 kwa ukiukwaji wa
maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais.
Kikao kilichopita cha CC kilichoketi Januari 13,
mwaka huu kilibainisha kuwa baada ya muda wa adhabu zao kuisha, Kamati
Kuu ingefanya tathimini kuona iwapo wagombea hao walizingatia masharti
ya adhabu zao na endapo kungekuwa na ambao hawakuzingatia masharti
adhabu zao zingeongezwa.
Wiki iliyopita, Nnauye alithibitisha kuwa muda wa
adhabu hiyo ulikuwa ukingoni na kuwa viongozi hao wangefanyiwa tathmini
na kamati ndogo ya maadili ili kubaini iwapo adhabu hiyo ilitekelezwa
ipasavyo.
Makada waliokuwa wakitumikia adhabu hiyo ni Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen
Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kikao hicho huenda pia kikazungumzia mwenendo wa
uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu kwa kutumia
teknolojia ya alama za vidole (BVR), iliyozinduliwa jana na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda.
CCM, ni miongoni mwa vyama vya siasa nchini
vinavyoungana na vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa),
kuhoji mara kwa mara ufanisi wa mfumo wa BVR katika kuandikisha
wapigakura kutokana na historia yake isiyoridhisha.
No comments:
Post a Comment