Ilikuwa ni kama marudio ya ajali ya mwaka 2002, lakini ukubwa wa athari za tukio la jana unatofautiana baada ya watu watatu kufariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuchota mafuta kutoka kwenye lori lililopinduka katika Kijiji cha Idweli.
Lori hilo lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Malawi,
lilipinduka kwenye milima ya Mporoto, eneo ambalo ajali kama hiyo
ilitokea mwaka 2002 na kuua watu 40 na wengine 100 kujeruhiwa na moto
uliolipuka wakati wanakijiji wakijaribu kuiba mafuta kutoka kwenye lori
hilo.
Usiku wa kuamkia jana, hali ilikuwa kama hiyo
katika Kijiji cha Idweli, Rungwe wakati lori jingine lilipolipuka kwenye
Barabara ya Mbeya-Malawi.
Katika tukio hilo, watu watatu walifariki dunia na
wengine 18 kujeruhiwa kwa moto uliowafuata hadi kwenye nyumba zao
walikoficha mafuta waliyoiba kutoka kwenye lori hilo.
Ofisa Tabibu wa Hospitali ya Igogwe, Alexanda
Masaru alisema alipokea miili miwili ya watu na mmoja alifariki wakati
akipatiwa matibabu na wengine 16 walilazwa baada ya kuungua sehemu
mbalimbali.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ahmed Msangi
aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Maria Pajela (18) na William
Paschal (38) wote wakazi wa Kijiji cha Idweli na utingo wa gari hilo
Frank Chaula.
Waliojeruhiwa ni Shukuru Kanzale (21), Nuru George
(30), Asante Boniface (38), Joseph Jamson (18), Joseph Paschal (30),
Siza Kinesa (22), Alex Daud (35), Oscar Yosia (23), Traiphon Moasi (37),
Samson Mbwila (29).
Wengine ni Dora Michael (35), Veronica Elia (30),
Rabsen Ayub (26), Wasiwasi Spika (32), Asia Anon (20), Bahati Kyando
(23), Christopher Erasto (32) na Melisa Sanane (50) wote wakazi wa
Kijiji cha Idweli.
Majeruhi azungumza
Mmoja wa majeruhi aliyelazwa kwenye Hospitali ya Igogwe, Wasiwasi Spika alisema aliungua wakati akichota mafuta hayo.
Spika alisema chanzo cha moto ni mtu mmoja aliyeshika kibatari jirani na eneo la ajali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Idweli, Marcus Msomba
alisema aliwaonya wakazi hao kukaa mbali na lilipopinduka gari hilo
lakini hawakusikia.
No comments:
Post a Comment