Zanzibar
MWAKILISHI wa Magomeni visiwani Zanzibar, Salmin Awadhi Salmin (CCM),
amefariki dunia ghafla baada ya kuanguka katika kikao cha Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kilichokuwa kinafanyika katika ofisi kuu ya chama
hicho, Kisiwandui mjini Unguja.
Taarifa hiyo ilianza kuenea mjini Unguja jana saa 6 mchana, na hata
kuzua maswali kutoka kwa wananchi kuhusu utata wa kifo chake.
Salmin (57) ambaye pia alikuwa ni mnadhimu wa wawakilishi wa CCM na
mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho (CC), alikuwa mmoja wa wawakilishi
wanaopinga mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kutaka
wananchi waulizwe kama bado wanahitaji muundo huo wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar.
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu kifo cha mwakilishi huyo, Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar, Vua Ali Vuai, alisema kabla ya kufikwa na mauti,
alianguka ghafla wakati akitoka katika kikao hicho cha kawaida.
Alisema baada ya kuanguka viongozi na wanachama walimnyanyua na kumkimbiza Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu.
“Baada ya Salmin kuanguka, baadhi ya viongozi na wafanyakazi kwa haraka
walimbeba na kumpeleka katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya
matibabu na baada ya kufikishwa alipelekwa katika chumba cha wagonjwa
mahututi (ICU), ambako baada ya muda mfupi madaktari walithibitisha kuwa
amefariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la damu.
“CCM imepokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha kiongozi wetu ambaye alikuwa
ni kiongozi na mtendaji wa kuigwa ndani na nje ya chama chetu, ila kazi
ya Mungu haina makosa, jambo la kusikitisha amefariki akiwa katika
utendaji wa kazi za chama hapa ofisi kuu Kisiwandui,” alisema Vuai.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kwa sasa taratibu za mazishi
zinaandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na chama nyumbani kwake
Mpendae na anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Makunduchi Mkoa wa
Kusini Unguja saa 7 mchana.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wawakilishi (BLW), Yahya Khamis
Hamad, alisema baraza hilo limeondokewa na kiongozi mahiri ambaye muda
wote alikuwa na kazi ya kuimarisha umoja kwa Wazanzibari.
Salmin Awadh Salmin alizaliwa mwaka 1958 kisiwani Unguja na kusoma Shule
ya Msingi Makunduchi kabla ya kuwa kiongoni Wilaya ya Kusini Unguja.
Pia amewahi kushika wadhifa mbalimbali ndani ya CCM ikiwamo ujumbe wa
NEC, Kamati Kuu na Mnadhimu wa Wawakilishi wa Kambi ya CCM ndani ya
Baraza la Wawakilishi.
Machi 2, mwaka jana wakati wa mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba mjini
Dodoma, Salmin aliwaongoza wawakilishi wa CCM kupinga hatua ya Spika wa
Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, kuwasilisha maoni kwa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya kutaka Serikali tatu na
kuyaita ni maoni ya baraza hilo.
Katika mkutano huo, Salmin alisema mapendekezo hayo ni kinyume na
msimamo wa CCM na wao hawako tayari kuliona hilo huku akiahidi suala
hilo kufikishwa katika vikao vya ngazi za juu.
Salmin alisema Spika Kificho hakuwashirikisha wenzake katika mapendekezo
ya Serikali tatu aliyoyawasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
wakisema Baraza la Wawakilishi, kama taasisi, halikutoa msimamo wa
pamoja.
Mei 4, mwaka jana, Salmin alisema wawakilishi wa CCM wanajiandaa
kuwasilisha hoja binafsi kwenye Baraza la Wawakilishi ili kuwapa nafasi
wananchi waulizwe iwapo wanataka kuendelea na Serikali ya Umoja wa
Kitaifa (SUK), au la.
Kauli hiyo aliitoa wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho
ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana kwenye viwanja vya
Kibandamaiti, Unguja.
Salmin alisema wajumbe hao wamefikia hatua hiyo kwa kuwa wanaona kwamba
lengo na matumaini ya kuundwa SUK yamefutika na hayana dalili njema
katika siku za usoni.
Alisema ni vyema wananchi wakaulizwa kama bado wana hamu na mfumo huo au ule wa zamani urejeshwe.
Katika mkutano huo, alimwomba Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein,
kuunga mkono hoja hiyo itakapowasilishwa ili kutoa nafasi mpya ya
kidemokrasia kwa wananchi wake kujua kama wanataka mfumo wa sasa au wa
zamani.
No comments:
Post a Comment