Polisi wa wa kituo cha Ilula kilicho Kilolo mkoani Iringa wanatuhumiwa kuua mtu mmoja, jambo lililoamsha vurugu kubwa zilizosababisha magari mawili kuchomwa moto.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa wananchi
waliokuwa na hasira walichoma moto magari yaliyokuwa yameegeshwa
kituoni hapo na kuchana nyaraka zilizokuwapo ndani pamoja na kufungulia
mahabusi.
Mapigano hayo kati ya polisi na wananchi yalitokea
wakati polisi wakifanya operesheni ya kukamata watu wanaokunywa pombe
muda wa kazi na kusababisha purukushani kubwa.
Mmoja wa mashuhuda hao, Omary Kivade, ambaye ni
mkazi wa Ilula, alisema kuwa polisi mmoja alionekana akimfukuza mwanamke
ambaye walimtuhumu kuwa alipika pombe wakati wa kazi. Alisema baada ya
polisi huyo kurudi, wananchi walishangaa kuona hakuwa amemkamata yeyote
na ndipo wakaamua kwenda kuangalia sehemu walikokimbilia na kumkuta
mwanamke huyo akiwa ameshafariki.
Alisema kufariki kwa mwanamke huyo kulipandisha
hasira wananchi ambao walirudi kituoni ambako walipindua magari manne na
kuchomo moto matatu madogo, basi aina ya Toyota Hiace, na pikipiki moja
katika vurugu hizo zilizodumu kwa saa tano.
Vurugu hizo zilisababisha barabara kuu ya Dar es
Salaam-Iringa kufungwa kwa takribani saa tano, kutoka saa 5:00 asubuhi
hadi saa 10:00 jioni.
Haikuweza kufahamika mara moja ni nini hasa
kimesababisha kifo cha mwanamke huyo kati ya kupigwa na polisi au
kuanguka wakati akimkimbia polisi asimkamate.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mkazi wa Ilula,
Jamila Athuman alisema baaada ya vurugu kutokea klabuni na wananchi
kusikia kuwa kuna mwenzao amekufa, walijikusanya na kuchoma matairi
barabarani na kusababisha magari kushindwa kupita.
Aliongeza kuwa polisi wa kituo cha Ilula
walizidiwa nguvu na wananchi waliokwenda kituoni hapo na watu hao
walichoma magari, kuwapiga askari waliokuwepo kituoni hapo.
Pia basi la kampuni ya Nyagawa linalofanya safari
zake kati Njombe na Dar es Salaam lilivunjwa vioo vyote na wananchi
baada ya askari kukimbilia kwenye basi hilo kuokoa maisha yao kutokana
na kuzidiwa nguvu na wananchi.
Alisema baada ya hali kuwa ya hatari, polisi wa
kijiji cha jirani kata ya Mbigili na Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)
Iringa walifika na kutuliza hali hiyo na barabara kurejea katika hali ya
kawaida.
Mmoja wa mashuhuda waliokuwapo eneo la tukio,
James Kilovela alisema baada ya polisi hao kufika eneo la tukio na
kuwatimua watu kwenye vilabu bila kutoa maelezo yoyote, wananchi
walianza kukimbia ovyo kuepuka kukamatwa.
No comments:
Post a Comment