Saturday, 21 February 2015

MUKANGARA AMSHAMBULIA LOWASSA .. AKANA TATIZO LA AJIRA KUA BOMU ...

 
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mkangara, amemshambulia kwa maneno makali Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na wanasiasa wengine wanaosimama majukwaani na kudai vijana ni bomu linalosubiri kulipuka.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika hafla ya kutia saini ya makubaliano ya kuwa na uhusiano wa utendaji kati ya wizara hiyo na Taasisi ya Kutoa Elimu ya Ujasiriamali (Esami), Dk. Mkangara, alisema kauli za namna hiyo ni za ovyo, zinamkera na zimejaa upuuzi kwa sababu vijana ni Taifa la leo na kesho linalohitaji kusaidiwa na si kuwakejeli.

Lowassa amewahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema ukosefu wa ajira kwa vijana ni bomu litakalolipuka wakati wowote ingawa kuna baadhi ya wanasiasa wamewahi kuipinga kauli yake.


Mbali na Lowassa, pia kauli ya namna hiyo imewahi kutolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.


Dk. Mkangara alisema vijana wanahitaji kupata ushauri mzuri na endelevu badala ya kuwakejeli kuwa ni bomu linalosubiri kulipuka.


“Kwanza sasa masuala ya kusema maneno ya kipuuzi hayatakiwi kwa kuwa vijana ndiyo Taifa la leo na kesho na linahitaji kusaidiwa na sio kuwakejeli.
“Viongozi wanaosimama na kusema kwamba vijana ni bomu linalosubiri kulipuka, ni watu wa ovyo ovyo na wananikera,” alisema Dk. Mkangara.


Alisema vijana wakitumiwa vizuri wanaweza kujihusisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kuweza kukuza uchumi wa nchi.


Katika hatua nyingine, alisema uhusiano waliouanzisha na Esami una lengo la kuwajengea uwezo vijana katika shughuli za kujiajiri huku akisisitiza kuwa ujasiriamali ni jambo muhimu katika kipindi hiki chenye changamoto ya ukosefu wa ajira.


“Kwa takwimu zilizopo, ukosefu wa ajira kwa kundi la vijana nchini ni asilimia 13.4 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012. Hivyo mradi huu utaiwezesha Serikali kupiga hatua katika kutekeleza mkakati wa kuwajengea vijana uwezo wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini,” alisema Dk. Mkangara.


Alisema ulimwengu wa sasa umekuwa na tabia ya mabadiliko ya mara kwa mara ya uchumi, siasa pamoja na mazingira yasiyotarajiwa.


Aliwataka vijana kutumia ubunifu na fikra pevu ili kujikwamua kiuchumi.
Awali, aliwataka vijana waachane na mtazamo wa kusoma kwa lengo la kuajiriwa na badala yake wasome ili kujiajiri na wakabiliane na ugumu wa maisha.


Alisema mradi wa Esami utatekelezwa nchi nzima na jumla ya dola milioni 15.44 za Marekani zinatarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza ya mradi huo.


Alisema wizara yake ina vituo vitatu vya mafunzo kwa vijana ambavyo ni Ilonga, Marangu na Mbeya na vitatumika kuwajengea vijana uthubutu, ubunifu, pamoja na darasa la kilimo, uvuvi na ICT.


Naye, Mkurugenzi wa Esami, Bonal Mwape, alisema watahakikisha wanashirikiana na Serikali kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri kupitia ujasiriamali.

No comments:

Post a Comment