Tuesday, 7 April 2015

MASHIRIKA YA KIRAIA KENYA YATAZAMIWA KUFANYA MAANDAMANO ..>>

 Mabweni ya Chuo kikuu cha sheria cha Nairobi ambapo Abdirahim Abdullahi alisomea.

Wanaharakati wa mashirika ya kiraia nchini Kenya wanatazamiwa kufanya maandamano Jumanne wiki hii wakipinga kile wanachokiita kutowajibika kwa vyombo vya usalama, baada ya shambulio dhidi ya Chuo kikuu cha Garissa Juma lililopita.


Katika shambulio hilo watu 148 ikiwa ni pamoja na wanafunzi 142 waliuawa, na wengine wengi walijeruhiwa.

Maandamano hayo yanakuja kwa siku ya tatu ya maombolezo, wakati ambapo vilio vimekua vikiongezeka baada ya familia kuwatambua ndugu zao.

Wingu la huzuni limeendelea kutanda kote nchini Kenya, hasa katika jiji la Nairobi ambapo zoezi la kuhuzunisha la kutambua wanafunzi waliouawa na magaidi wa Al Shabab likiendelea.

Wanafunzi walionusurika wameendelea kutoa ushuhuda wao kuhusu tukio hilo na mbinu walizotumia ili kunusurika.

Hali ya huzuni imeendelea kutanda nchini Kenya, kila mmoja akiendelea kumkumbuka ndugu yake aliepoteza maisha katika shambulio hilo.

Wakati huohuo, mkurugenzi wa kituo cha kurasibu majanga ameahidi kuanzisha haraka iwezekanavyo zoezi la kutambua miili ya wahanga wa shambulio la Chuo kikuu cha Garissa, kaskazini mwa Kenya. Tangu Ijumaa wiki iliopita, familia za wahanga kutoka nchi nzima wamejielekeza Nairobi ili kujua hatima ya ndugu zao.

Hayo yakijiri, baada ya siku kuu ya Pasaka, Jumapili mwishoni mwa juma lililopita, wanafunzi wa Chuo kikuu katika kitivo cha sheria mjini Nairobi wameanza kurejea katika mabweni. 

Mazungumzo yao yamejikita hasa katika shambulio dhidi ya Chuo kikuu cha Garissa. Mmoja wa washambuliaji aliye tambuliwa na viongozi aliwahi kusomea kwenye Chuo kikuu cha Garissa na kupata shahada katika sheria. Abdirahim Abdullahi alihitimisha elimu yake kwenye Chuo kikuu hicho mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment