JOHNSON MINJA
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Johnson Minja amesema hakuna dalili zinazoonyesha kuwa mgogoro uliopo kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) utaweza kumalizwa na Serikali iliyopo madarakani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake
mwishoni mwa wiki, Minja alisema baadhi ya viongozi waliopo madarakani
wanashindwa kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro huo kwa kuwa
wananufaika na biashara ya kuuza mashine za risiti za kieletroniki (EFD)
ambazo zinapingwa na wafanyabiashara.
Pia, mwenyekiti huyo alisema kuwa viongozi hao
wanajinufaisha kutokana na mapato yanayopatikana kwenye kodi inayolipwa
kwa njia isiyo sahihi.
Akifafanua Minja alisema tangu kuingizwa kwa
mashine za EFD nchini, kumekuwapo na ‘misuguano’ kati ya wafanyabishara
na TRA kwa kuwa mashine hizo zinakata kodi kwenye mauzo ya bidhaa na si
kwenye faida kama ilivyo kwenye mashine za aina hiyo katika nchi
nyingine.
Akitoa mfano, Mwenyekiti huyo alisema: “Ukienda
kununua sahani ya ndizi ambayo inauzwa Sh10,000 ile mashine ya EFD
ukiitumia itaonyesha mauzo ya bidhaa hiyo kwa Sh10,000, lakini mpaka ile
sahani ikafika mezani ina maana kwamba ulinunua ndizi, nyama, nyanya,
vitunguu na mafuta lakini hakuna namna ya kuweza kupata uthibitisho wa
stakabadhi kwenye vitu vyote ulivyovinunua.”
Alisema kwamba kwa Sheria ya Mapato, kodi inayopaswa kukatwa ni asilimia 30 ya ile Sh10,000 ambayo ni sahani moja ya ndizi, ingawa mfanyabiashara hakupata faida hata Sh1,000.
Minja ambaye kitaaluma ni mhasibu, aliongeza kuwa
wafanyabiashara wanahoji namna ambavyo Serikali ilifikia uamuzi wa kuuza
mashine za EFD kwa Sh800,000 wakati bei yake halisi haizidi Sh50,000.
“Tulipowauliza (TRA) walituambia mashine za EFD
zinazotumika Tanzania hazipatikani sehemu nyingine yoyote ulimwenguni,
lakini ukilinganisha na tulizo nazo sisi zinatofautiana sehemu ya kuweka
kadi tu,” alisema.
Huku akionyesha kujiamini, mwenyekiti huyo alidai
kuwapo kwa njia mbili za kulipa bidhaa zinazochukuliwa bandarini,
utaratibu ambao unawanufaisha baadhi ya vigogo nchini.
Akitoa mfano wa kuingiza kontena bandarini, Minja,
alisema: “Ukitaka kulipa mwenyewe utajikuta unaambiwa kodi ni Sh200
milioni lakini kuna watu fulani ukiwatumia ambao wana uhusiano na watu
fulani bandarini utalipa Sh40 milioni lakini utapewa stakabadhi ya Sh10
milioni.
“Sasa mtu ataenda wapi, akalipe Sh200 milioni au
Sh40 milioni akapewe stakabadhi ya Sh10 milioni? Wote watakwenda kwenye
Sh10 milioni halafu anapotakiwa kuonyesha gharama zake zilizotumika
hataweza kuionyesha ile Sh40 milioni kwa sababu stakabadhi aliyonayo ni
Sh10 milioni,” alisema.
No comments:
Post a Comment