Monday, 16 February 2015

AZAM YAIZIMA EL MERREIKH ...>>>


Mabingwa wa Tanzania Bara, Azam FC wameanza kwa kishindo Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuichapa El Merreikh kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mshambuliaji Didier Kavumbagu alifungia Azam bao la kuongoza dakika ya 9, kabla ya nahodha John Bocco aliyeingia akitokea benchi kupachika bao la pili kwa mabingwa hao wa Tanzania na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele kabla ya mchezo wa marudiano.
Ushindi huo wa Azam umekuja ikiwa ni siku moja baada ya wawakilishi wengine wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho, Yanga kuichapa BDF XI kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
El Merreikh ilianza mchezo kwa kasi na kufanikiwa kupata kona mbili katika dakika tano za mwanzo, lakini hazikuzaa matunda.
Azam walijibu mapigo dakika ya nne wakati shuti la Kipre Tchetche lilipodakwa kwa umakini na kipa wa El Merreikh, Magoola Salim dakika ya nne na saba.
Kinara wa ufungaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara,  Kavumbagu aliwainua mashabiki wa Azam katika dakika ya tisa kwa kufunga bao la kuongoza akiunganisha krosi iliyoshindwa kuokolewa na beki Silomon Jabson, ukamkuta Kavumbagu aliyepiga shuti lililookolewa na kipa Salim na kurudi tena kwa Mrundi huyo na mara ya pili hakufanya ajizi.
Baada ya bao hilo, Azam ilirudi mchezoni na kuanza kucheza kwa kujiamini, lakini washambuliaji wake Tchetche, Kavumbagu pamoja na viungo wake Frank Domayo, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ walishindwa kutumia vizuri nafasi nyingi walizozipata.
Wakati washambuliaji wakipoteza nafasi, mabeki wa Azam, Pascal Wawa, Aggrey Morris, Shomari Kapombe na kipa Aishi Manura walifanya kazi ya ziada kuwazuia nyota wa El Merreikh, Watende Allan, Kortokaila Balla na Abdalla Ragei. Kipindi cha pili, El Merreikh iliingia kwa kasi na kulishambulia kama nyuki lango la Azam, lakini ukuta wa Azam ulikuwa makini kuzuia mashambulizi yote ya Wasudani hao.
Azam iliwampumzisha Domayo na kumwingiza Himid Mao kabla ya kumtoa Tchetche na kumwingiza Bocco aliyeingia akitokea benchi na kuifungia Azam bao la pili akiunganisha kwa kichwa mpira uliorushwa na Nyoni ambao uligongwa kichwa na Kavumbagu na kumkuta Bocco aliyepiga kichwa na kujaza wavuni dakika 77.
Kocha wa Azam, Joseph Omog amewasifu wachezaji wake kwa kucheza kwa umakini na kupata matokeo hayo.
“Tunatakiwa kucheza kwa umakini zaidi katika mchezo wa marudiano ili kutimiza lengo letu la kusonga mbele, mechi ijayo itakuwa ngumu zaidi.”
Azam: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Michael Boluo, Salum Abubakari, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche, na Brian Majengwa.

No comments:

Post a Comment