Ghana na Ivory Coast ndio zitakutana katika fainali ya kombe la
mataifa Afrika 2015 Jumapili, Februari 8 mjini Bata. Ghana ilijikatia
tiketi ya fainali kwa kuwachapa wenyeji Equatorial Guinea 3-0 katika
mechi ya pili ya nusu fainali Alhamisi.
Ivory Coast ndio ilikuwa ya kwanza kuingia fainali baada ya kuichapa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - DRC - 3-1 katika nusu fainali ya
kwanza Jumatano.
Ghana ilipata bao la kwanza katika mechi yao dhidi ya Equatorial
Guinea kwa njia ya penalti katika dakika ya 42 pale Jordan Ayew
alipachika penalti ya kiulaini kabisa baada ya golikipa kumvamia
mshambuliaji wa Ghana.
Dakika chache baada kabla ya halftime Wakaso aliipatia Ghana bao la
pili baada ya kupokea krosi nzuri ambayo alidhibiti kwa guu la kulia na
kumwacha mlinzi wa Equatorial Guinea kando na kupachika bao safi
kimiani.
Katika nusu ya pili Equatorial Guinea walinza kuonekana
kuchanganyikiwa kwa uchezaji wa hasira hapa na pale na hali hiyo
ilifungua fursa nyingine kwa Ghana kupata bao la tatu katika dakika ya
75 ambalo lilifungwa na Andre Ayew.
Mechi ilisimamishwa kwa dakika kadha zikiwa zimebaki kiasi cha dakika
saba kutokana na ghasia zilizoanzia katika stendi wa watizamaji ambao
inaelekea walikuwa wakitupa chupa na mawe uwanjani. Baada ya muda mchezo
ulirejea uwanjani lakini hadi wakati huo mshindi alikuwa wazi.
Wachambuzi wa kandanda Afrika wanasema fainali hii ni ile ambayo
wamekuwa wakiotea kwa muda mrefu baina ya Ghana na Ivory Coast - timu
ambazo zina wachezaji kadha katika ligi za Ulaya.
No comments:
Post a Comment