Sunday, 8 February 2015

MOTO ULIOUA FAMILIA YA WATU SITA WAZUA MAPYA DAR ...>>

Waombolezaji kwenye msiba uliotokana na ajali ya moto ulioteketeza watu sita wa familia moja, wamelaumu Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushindwa kufika kwa wakati eneo la tukio.

Juzi familia ya watu sita ya Mzee David Mpira na mkewe Celina, iliteketea kwa moto ikijumuisha Lucas Mpira, Samwel Yegela, Pauline Emmanuel na Celina Emmanuel. Chanzo cha moto huo inadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.
Katika tukio hilo, Emmanuel Mpira ndiye pekee aliyenusurika katika ajali hiyo kwa kuwa wakati moto unatokea yeye alikuwa ametoka kwenda matembezini.
Jana, waombolezaji hao ambao wengi ni wakazi wa Kipunguni A ilipoteketea nyumba hiyo, kwa nyakati tofauti walisema hakuna haja ya kuwepo kikosi hicho ambacho mara kwa mara kimekuwa kikifika kimechelewa kwenye maeneo ya matukio ya ajali na hata kama wakiwahi wanakuwa hawana maji.  “Tumepiga simu tangu saa 10.00 usiku mara baada ya kuona moto unateketeza nyumba lakini wamefika hapa saa 12.00 asubuhi wakati moto umeshateketeza kila kitu,” alisema Abdallah Mlele mkazi  wa eneo hilo.
Mlele alikuwa akiungwa mkono na wenzake ambao walisema kwa utendaji unaonyeshwa na chombo hicho ni bora kisiwepo.
“Hakuna haja ya kuwapigia simu ‘fire’ wakati wanakuja kuzima moto wakiwa wamechelewa na wakati mwingine hawana maji,” alisema.
Akizungumzia hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya ambaye ni ndugu wa familia hiyo, alisema si vizuri kuzungumzia suala hilo katika kipindi hiki bali kinachotakiwa ni kusubiri uchunguzi.

No comments:

Post a Comment