Zanzibar. Mustakabali wa
uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), upo shakani
kutokana na wananchi kutofautiana kuhusu umuhimu wa kuendelea na mfumo
huo wa uongozi, huku baadhi wakitaka iitishwe Kura ya Maoni kuamua hatma
ya serikali hiyo.
SUK iliundwa mwaka 2010 baada ya vyama vikuu vya
siasa visiwani hapa, CCM na CUF, kujadiliana na hatimaye kufikia muafaka
wa kugawana madaraka ili kuondoa siasa za chuki zilizotokana na
machafuko ya mwaka 2005 wakati wananchi walipokuwa wakipinga matokeo ya
Uchaguzi wa Rais.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwananchi
unaonyesha kuwa iwapo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) haitakuwa
makini katika usimamiaji wa kanuni na sheria za uendeshaji wa kampeni
hadi kuelekea Uchaguzi Mkuu, kuna uwezekano mkubwa wa wanasiasa wa pande
mbili kuyatumia vibaya majukwaa na kuiparaganyisha serikali hiyo.
Tatizo jingine linaloonekana kuinyemelea SUK ni kuibuka kwa watu
wanaotaka ifanyike Kura ya Maoni na wananchi kuulizwa kama wanataka
mfumo huo wa uendeshaji serikali kwa pamoja unastahili kuendelea.
Kutoimarika kwa huduma za jamii chini ya SUK kama
ilivyotegemewa na wananchi na malengo yake kutofikiwa kunaelezwa pia
kuwa ni kati ya changamoto zinazoikabili SUK.
Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini ya Jumuiya ya Asasi za Kiraia Zanzibar (Angoza), Mohamed
Hafidh Khalfan alitetea SUK akisema kwamba faida zimeonekana, ikiwamo
kudumishwa kwa amani na kuondoa mgawanyiko katika jamii, lakini akasema
yapo mambo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ya msingi kulinda ustawi
wa serikali hiyo.
Khalfan alisema viongozi wa juu wa SUK bado
wanaona kwamba mfumo huo wa uendeshaji Serikali ni miliki yao binafsi
isiyohusisha wananchi. “Ndani ya mwaka mmoja, wananchi walitakiwa kupewa
elimu ya uraia kuhusu SUK kwa kuzishirikisha asasi za kiraia; Serikali
imewaacha wananchi wakigawanyika na kuwa na ufahamu mdogo wa mfumo
wenyewe. Hili ni tatizo linalotishia uhai na mustakabali wa jambo hilo,”
alisema Khalfan. Pia alisema kuwa kwa miaka minne, SUK imeshindwa
kuleta na kuibua mabadiliko ya msingi serikalini kutokana na makatibu
wakuu, makamishna, wakuu wa mikoa na wilaya kubaki watu wale wale huku
wakiteuliwa kwa kuangaliwa itikadi zao kisiasa na kushindwa kusukuma
uwajibikaji na utendaji wenye tija.
Kamishna mstaafu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Simai Mohamed Said alieleza kuwa bado SUK ina umuhimu mkubwa licha ya
kujitokeza baadhi ya watu kuipinga bila ya kuwa na nguvu ya hoja na
kutojali kuhesabu mema yaliyopatikana, huku wakitoa kasoro haba
zinazoweza kufanyiwa marekebisho ya msingi.
Simai alisema uhai wa SUK umetokana na hekima, uongozi bora na siasa safi ya Dk Shein katika kusimamia Serikali kisera.
Alisema zipo faida lukuki zilizopatikana tangu
kuundwa kwa mfumo huo, ikiwa ni pamoja na wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar bila kujali itikadi zao za kisasa, kuikosoa
serikali kila inapoteleza au kujisahau.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Serikali Zanzibar
(Suza), Ali Haji Vuai alisema malengo ya SUK kimsingi yalikuwa matatu,
moja ikiwa ni kuondoa hofu ya kisiasa.
Vuai anasema SUK imeishia katika hatua moja kati
ya hizo, ambayo aliitaja kuwa ni kuiunganisha jamii kutokana na chuki za
kisiasa, lakini akakosoa ujenzi na utendaji wa uendeshaji serikali
hiyo, akisema bado haujabadilika kutokana na nyadhifa nyingi za
watendaji wakuu kunufaisha upande mmoja.
Alisema kosa kubwa ni kukosekana kwa imani ya
pamoja na badala yake vyama viwili vinaunda Serikali moja ambayo
inatekeleza sera ya chama kimoja.
No comments:
Post a Comment